Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Yohana 6:16-51 in Swahili (individual language)

Help us?

Yohana 6:16-51 in Biblia Takatifu

16 Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,
17 wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado.
18 Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.
20 Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!”
21 Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walipokuwa wanakwenda.
22 Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao.
23 Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.
24 Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
25 Wale watu walipomkuta Yesu ng'ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?”
26 Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27 Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uzima wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.”
28 Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?”
29 Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini yule aliyemtuma.”
30 Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?
31 Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.”
32 Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni.
33 Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uzima.”
34 Basi, wakamwambia, “Mheshimiwa, tupe daima mkate huo.”
35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
36 Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.
37 Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,
38 kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.
39 Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho.
40 Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho.”
41 Basi, Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
42 Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?”
43 Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika ninyi kwa ninyi.
44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho.
45 Manabii wameandika: Watu wote watafundishwa na Mungu. Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.
46 Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
47 Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
50 Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa.
51 Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
Yohana 6 in Biblia Takatifu

Yohana 6:16-51 in Biblia ya Kiswahili

16 Ilipokuwa jioni, wanafunzi wake walishuka kwenda ziwani.
17 Wakapanda kwenye mtumbwi na walikuwa wakivuka kuelekea Kapernaumu. (Giza lilikuwa limeingia na Yesu alikuwa bado hajaja kwao).
18 Wakati huo upepo mkali ulikuwa ukivuma, na bahari ilikuwa ikendelea kuchafuka.
19 Tena wanafunzi wake walipokuwa wamepiga makasia kama ishirini na matano au thelathini, wakamwona Yesu akitembea juu ya bahari kuukaribia mtumbwi, na wakaogopa.
20 Lakini akawambia, “Ni mimi! Msiogope.”
21 Tena walikuwa tayari kumbeba kwenye mtumbwi, na mara mtumbwi ulifika kwenye nchi mahali walipokuwa wakienda.
22 Siku iliyofuata, mkutano uliokuwa umesimama upande wa bahari waliona kuwa hakuna mtumbwi mwingine isipokuwa ule ambayo Yesu na wanafunzi wake walikuwa hawajaupanda lakini wanafunzi wake walikuwa wameenda zao wenyewe.
23 (Ingawa, kulikuwa na baadhi ya mitumbwi iliyotoka Tiberia karibu na mahali walipokula mikate baada ya Bwana kutoa shukrani).
24 Wakati makutano walipotambua kuwa sio Yesu wala wanafunzi wake walikuwa kule, wao wenyewe walipanda ndani ya mitumbwi wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.
25 Baada ya kumpata upande mwingine wa ziwa wakamuuliza, “Rabbi ulikuja lini huku?”
26 Yesu akawajibu, akawambia, Amini, amini, mnanitafuta mimi, sio kwa sababu mliziona ishara, bali kwa sababu mlikula mikate na kushiba.
27 Acheni kukifanyia kazi chakula chenye kuharibika, bali mkifanyie kazi chakula kidumucho hata milele kile ambacho mwana wa Adamu atawapa, kwa kuwa Mungu Baba ameweka muhuri juu yake.”
28 Kisha wakamwambia, “Ni nini tunapaswa kufanya ili kuzifanya kazi za Mungu?”
29 Yesu akajibu, “Hii ndiyo kazi ya Mungu: kwamba mmwamini yeye aliyemtuma.”
30 Basi wakamwambia, “Ni ishara zipi utakazofanya, kwamba tunaweza kuziona na kukuamini? Utafanya nini?
31 Baba zetu walikula manna jangwani, kama ilivyo andikwa, “Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.”
32 Kisha Yesu akawajibu, “Amini, amini, sio Musa aliyewapa mkate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye awapaye mkate wa kweli kutoka mbinguni.
33 Kwa kuwa mkate wa Mungu ni ule ushukao kutoka mbinguni na kuupatia uzima ulimwengu.
34 Basi wakamwambia, “Bwana tupatie huu mkate wakati wote.”
35 Yesu akawambia, “Mimi ndiye mkate wa uzima, yeye ajaye kwangu hatapata njaa na yeye aniaminiye hatahisi kiu kamwe.”
36 Ingawa niliwaambia kwamba, mmeniona, na bado hamuamini.
37 Wote ambao Baba anaonipa watakuja kwangu, na yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kabisa.
38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni, sio kwa ajili ya kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma.
39 Na haya ndiyo mapenzi yake aliyenituma, kwamba nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali nitawafufua siku ya mwisho.
40 Kwa kuwa haya ndiyo mapenzi ya Baba yangu, kwamba yeyote amtazamaye Mwana na kumwamini apate uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
41 Kisha wayahudi wakamnung`unikia kumhusu yeye kwa sababu alisema, “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
42 Wakasema, “Huyu siyo Yesu mwana wa Yusuph, ambaye baba yake na mama yake tunamfahamu? Imekuwaje sasa anasema, 'Nimeshuka kutoka mbinguni`?”
43 Yesu akajibu, akawambia, “Msinung'unikiane miongoni mwenu wenyewe.
44 Hakuna mtu ajaye kwangu asipovutwa na Baba yangu aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.
45 Kwa kuwa imeandikwa katika manabii, 'Watafundishwa na Mungu.' Kila aliyesikia na amejifunza kutoka kwa Baba, huja kwangu.
46 Sio kwamba kuna mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu- amemwona Baba.
47 Amini, amini yeye aaminiye anao uzima wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 mababa zenu walikula manna jangwani, na wakafa.
50 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, ili kwamba mtu aule sehemu yake ili asife.
51 Mimi ni mkate uishio ambao umeshuka kutoka mbinguni. Kama mtu yeyote akila sehemu ya mkate huu, ataishi milele. Mkate nitakao utoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
Yohana 6 in Biblia ya Kiswahili