28 Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,
29 “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?”
30 Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
31 Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, ule chakula.”
32 Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.”
33 Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?”
34 Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
35 Ninyi mwasema: Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika! Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.
36 Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
37 Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: Mmoja hupanda na mwingine huvuna.
38 Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao.”
39 Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.”
40 Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili.
41 Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.
42 Wakamwambia yule mama, “Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu.”
43 Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya.
44 Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, “Nabii hapati heshima katika nchi yake.”
45 Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
46 Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu.
47 Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi.
48 Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!”
49 Huyo ofisa akamwambia, “Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.”
50 Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao yu mzima.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
51 Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima.
52 Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, “Jana saa saba mchana, homa ilimwacha.”
53 Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: “Mwanao yu mzima.” Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.