19 Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, “Amani kwenu!”
20 Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana.
21 Yesu akawaambia tena, “Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi.”
22 Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu.
23 Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowaondolea, hawasamehewi.”
24 Thoma mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja.
25 Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Thoma akawaambia, “Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki.”
26 Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, “Amani kwenu!”