19 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: “Wewe u nani?”
20 Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”
21 Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”
22 Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”
23 Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana.”
24 Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25 Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?”
26 Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
27 Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
29 Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30 Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!
31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.”
32 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
33 Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
34 Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
35 Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
36 Alipomwona Yesu akipita akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu.”
37 Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.