11 (Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: “Ninyi mmetakata, lakini si nyote.”)
12 Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, “Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?
13 Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi.
14 Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu.
15 Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni.
16 Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma.
17 Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
18 “Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.
19 Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi.
20 Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.”
21 Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!”
22 Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani.
23 Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.
24 Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.”
25 Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?”
26 Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
27 Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!”
28 Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.
29 Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini.