9 Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora zaidi kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi.
10 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu!
11 Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu.
12 Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.
13 Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka.
14 Vinywa vyao vimejaa laana chungu.
15 Miguu yao iko mbioni kumwaga damu,
16 popote waendapo husababisha maafa na mateso;
17 njia ya amani hawaijui.
18 Hawajali kabisa kumcha Mungu.”
19 Tunajua kwamba Sheria huwahusu walio chini ya Sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu.
20 Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuishika Sheria; kazi ya Sheria ni kumwonyesha tu mtu kwamba ametenda dhambi.
21 Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea Sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili.
22 Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote.
23 Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu.
24 Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa.
25 Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonyesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu;
26 lakini sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonyesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonyesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humkubali kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.