1 Anayependa mafundisho hupenda maarifa, bali yule anayechukia maonyo ni mpumbavu.
2 Yehova humpa fadhila mtu mwema, bali mtu ambaye hufanya mipango ya ufisada atahukumiwa.
3 Mtu hawezi kuimarishwa kwa uovu, bali wale watendao haki hawawezi kung'olewa.
4 Mke mwema ni taji ya mume wake, bali yule aletaye aibu ni kama ugonjwa unaoozesha mifupa yake.
5 Mipango ya wale watendao haki ni adili, bali shauri la mwovu ni udanganyifu.
6 Maneno ya watu waovu ni uviziaji unaosubiri nafasi ya kuua, bali maneno ya mwenye haki yatawatunza salama.
7 Watu waovu wametupwa na kuondolewa, bali nyumba ya wale watendao haki itasimama.
8 Mtu husifiwa kwa kadri ya hekima yake, bali yule anayechagua ukaidi hudharauliwa.
9 Bora kuwa na cheo duni- kuwa mtumishi tu- kuliko kujisifu kuhusu ukuu wako bila kuwa na chakula.
10 Yule atendaye haki anajali mahitaji ya mnyama wake, bali huruma ya mwovu ni ukatili.
11 Yule atendaye kazi katika shamba lake atapata chakula tele, bali anayesaka miradi duni hana akili.
12 Watu waovu hutamani wanavyoiba watu wabaya kutoka kwa wengine, bali tunda la wale watendao haki hutoka kwao mwenyewe.