Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Mathayo 13:24-58 in Swahili (individual language)

Help us?

Mathayo 13:24-58 in Biblia Takatifu

24 Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.
25 Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake.
26 Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.
27 Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, Mheshimiwa, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?
28 Yeye akawajibu, Adui ndiye aliyefanya hivyo. Basi, watumishi wake wakamwuliza, Je, unataka twende tukayang'oe
29 Naye akawajibu, La, msije labda mnapokusanya magugu, mkang'oa na ngano pia.
30 Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.”
31 Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake.
32 Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikishaota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, na ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”
33 Yesu akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga pishi tatu, hata unga wote ukaumuka.”
34 Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano,
35 ili jambo lililonenwa na nabii litimie: “Nitasema kwa mifano; nitawaambia mambo yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.”
36 Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani.”
37 Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu.
38 Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao Ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu.
39 Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika.
40 Kama vile magugu yanavyokusanywa kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati;
41 Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika Ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu,
42 na kuwatupa katika tanuru ya moto, na huko watalia na kusaga meno.
43 Kisha, wale wema watang'ara kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Sikieni basi, kama mna masikio!
44 “Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.
45 “Tena, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri.
46 Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile.
47 “Tena, Ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina.
48 Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa.
49 Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema,
50 na kuwatupa hao wabaya katika tanuru ya moto. Huko watalia na kusaga meno.”
51 Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.”
52 Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa Sheria aliye mwanafunzi wa Ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.”
53 Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo,
54 akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu?
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?
56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?”
57 Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!”
58 Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.
Mathayo 13 in Biblia Takatifu

Mathayo 13:24-58 in Biblia ya Kiswahili

24 Yesu aliwapa mfano mwingine. Akisema, “Ufalme wa mbinguni unafananishwa na mtu aliye panda mbengu nzuri katika shamba lake
25 Lakini watu waliposinzia, adui wake akaja pia akapanda magugu katikati ya ngano kisha akaenda zake.
26 Baadaye ngano ilipoota na kutoa mazao yake, ndipo magugu yalitokea pia.
27 Na watumishi wa mwenye shamba walikuja wakamwambia, 'Bwana, hukupanda mbengu nzuri katika shamba lako? Imekuwaje sasa lina magugu?
28 Akawaambia, Adui ametenda hili.' Watumishi walimwambia, “Kwa hiyo unataka twende tukayang'oe?”
29 Mwenye shamba akisema, 'Hapana, wakati mnayang'oa magugu mtang'oa pamoja na ngano.
30 Yaacheni yakue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati wa mavuno nitasema kwa wavunaji, 'Kwanza yang'oeri magugu na yafungeni matita matita na kuyachoma, lakini kusanyeni ngano katika ghala langu.''''
31 Kisha Yesu aliwatolea mfano mwingine. Akasema, “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake.
32 Mbegu hii kwa hakika ni ndogo kuliko mbegu zingine zote. Lakini imeapo huwa kubwa kuliko mimea yote ya bustani, huwa mti, kiasi kwamba ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”
33 Akawaambia mfano mwingine tena.” Ufalme wa mbinguni ni kama chachu ile iliyo twaliwa na mwanamke na kuichanganya kwa vipimo vitatu kwa unga mpaka viumuke.
34 Hayo yote Yesu aliyasema kwenye umati kwa mifano. Na pasipo mifano hakusema chochote kwao.
35 Hii ilikuwa kwamba kile kilichokwisha semwa kupitia kwa nabii kiweze kutimia, pale aliposema, “Nitafumbua kinywa changu katika mifano. Nitasema mambo yale yaliyokuwa yamefichwa tangu misingi ya ulimwengu”.
36 Kisha Yesu aliwaacha makutano na kwenda nyumbani. Wanafunzi wake walimwendea na kusema, “Tufafanulie mfano wa magugu ya shambani.''
37 Yesu alijibu na kusema, “Apandae mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu.
38 Shamba ni ulimwengu; na mbegu nzuri, hawa ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu, na adui aliye zipanda ni ibilisi.
39 Na mavuno ni mwisho wa ulimwengu, na wavunaji ni malaika.
40 Kama vile magugu yanavyo kusanywa na kuchomwa moto, hivyo ndivyo itakavyo kuwa mwisho wa ulimwengu.
41 Mwana wa Adamu atatuma malaika wake, na kukusanya kutoka katika ufalme wake mambo yote yaliyosababisha dhambi na wale watendao maasi.
42 Watawatupa wote katika tanuru la moto, ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.
43 Ndipo watu wenye haki watakapong'aa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio na sikie.
44 Ufalme wa mbinguni ni kama hazina iliyofichwa shambani. Mtu akaiona na kuificha. Katika furaha yake akaenda kuuza vyote alivyokuwa navyo, na kulinunua shamba.
45 Tena, ufalme wa mbinguni ni kama mtu anayefanya biashara atafutaye lulu yenye thamani.
46 Wakati alipoiona ile yenye thamani, alienda akauza kila kitu alichokuwa nacho na akainunua.
47 Ufalme wa mbinguni ni kama nyavu iliyo ndani ya bahari, na kwamba hukusanya viumbe vya kila aina.
48 Ulipojaa wavuvi waliuvuta ufukweni. Kisha wakakaa chini wakakusanya vitu vyema ndani ya vyombo, lakini visivyo na thamani vilitupwa mbali.
49 Itakuwa namna hii katika mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenga watu waovu kutoka miongoni mwa wenye haki.
50 Na kuwatupa ndani ya tanuru ya moto, ambako kutakuwa na maombolezo na kusaga meno.
51 Mmefahamu mambo yote haya? Wanafunzi walimjibu, ''Ndiyo.''
52 Kisha Yesu akawambia, ''Kila mwandishi ambaye amekuwa mwanafunzi wa ufalme anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.''
53 IkawaYesu alipomaliza mifano yote hiyo, akaondoka katika sehemu hiyo.
54 Kisha Yesu akafika katika mkoa wake na akawafundisha watu katika sinagogi. Matokeo yake ni kuwa walishangaa na kusema, “Ni wapi mtu huyu alipopata hekima hii na miujiza hii?
55 Mtu huyu siyo mwana wa seremala? Mariamu siyo mamaye? Na ndugu zake siyo Yakobo, Yusuph, Simoni na Yuda?
56 Na dada zake tunao hapa petu? Basi mtu huyu ameyapata wapi haya yote?”.
57 Aliwachukiza. Lakini Yesu aliwambia, “Nabii hakosi kuwa na heshima isipokuwa kwao na katika nchi yao.
58 Na hakuweza kufanya miujiza mingi kwa sababu hawakuwa na imani naye.
Mathayo 13 in Biblia ya Kiswahili