16 Ikawa kwamba, tulipokuwa tunaenda mahali pa kuomba, msichana mmoja aliyekuwa na pepo la utambuzi akakutana nasi. Alimletea bwana wake faida nyingi kwa kubashiri.
17 Mwanamke huyu alimfuata Paulo pamoja na sisi, akipiga kelele na kusema “Hawa wanaume ni watumishi wa Mungu aliye Mkuu, wanaowatangazia ninyi habari ya wokovu”.
18 Alifanya hivyo kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa amekasirishwa na tendo hilo, aligeuka nyuma na kumwambia pepo, “Nakuamuru kwa Jina la Yesu umtoke ndani yake.” Naye akatoka na kumwacha mara moja.
19 Mabwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limeondoka, waliwakamata Paulo na Sila na kuwaburuza sokoni mbele ya wenye mamlaka.
20 Walipowafikisha kwa mahakimu, walisema, “Hawa wanaume ni Wayahudi na wanasababisha ghasia kubwa katika mji wetu.
21 Wanafundisha mambo ambayo siyo sheria sisi kuyapokea wala kuyafuata kama Warumi.”
22 Umati ukawainukia kinyume Paulo na Sila, mahakimu wakararua nguo zao na kuwavua na kuamuru wachapwe viboko
23 Baada ya kuwachapa viboko vingi, waliwatupa gerezani na kumuamuru askari wa gereza kuwalinda vyema.
24 Baada ya kupokea amri hiyo, askari wa gereza aliwatupa katika chumba cha ndani ya gereza na kuwafunga miguu yao kwenye sehemu alipowahifadhi.
25 Wakati wa usiku wa manane, Paulo na Sila wakawa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwasikiliza,
26 Ghafla kukatokea tetemeko kuu na misingi ya gereza ikatikiswa, milango ya gereza ikafunguka, na minyororo ya wafungwa wote ikalegezwa.
27 Mlinzi wa Gereza aliamka kutoka usingizini na akaona milango yote ya gereza imefunguliwa; hivyo akachukua upanga wake maana alitaka kujiua kwa sababu alifikiri wafungwa wote walikwishatoroka,
28 Lakini, Paulo akapiga kelele kwa sauti kuu, akisema “usijidhuru kwa sababu wote tuko mahali hapa”.
29 Mlinzi wa gereza aliomba taa ziletwe na akaingia ndani ya gereza kwa haraka, akitetemeka na kuogopa, akawaangukia Paulo na Sila,
30 na kuwatoa nje ya gereza na kusema, “Waheshimiwa, nifanye nini ili nipate kuokoka?”
31 Nao wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”
32 Walinena neno la Bwana kwake, pamoja na watu wote wa nyumbani kwake,
33 Mlinzi wa gereza aliwachukua usiku ule na kuwaosha sehemu walizoumia, yeye pamoja na watu wa nyumbani mwake wakabatizwa mara.
34 Akawaleta Paulo na Sila nyumbani kwake na kuwatengea chakula. Naye akawa na furaha kuu pamoja na watu wa nyumbani mwake kwa sababu walimwamini Mungu.
35 Ilipokuwa mchana, mahakimu walituma ujumbe kwa yule mlinzi wa gereza wakisema, “Waruhusu wale watu waende”,
36 Mlinzi wa gereza akamjulisha Paulo juu ya maneno hayo ya kuwa, “Mahakimu walituma ujumbe niruhusu mwondoke: hivyo tokeni nje na mwende kwa amani.”
37 Lakini Paulo akawaambia, “Walitupiga hadharani, watu ambao ni Warumi bila kutuhukumu na waliamua kututupa gerezani; halafu sasa wanataka kututoa kwa siri? Hapana, haitawezekana, wao wenyewe waje kututoa mahali hapa”.