8 Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.
9 Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.
10 Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?
11 Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.”
12 Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.
13 Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: “Ndugu zangu, nisikilizeni!
14 Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.
15 Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
16 Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena.
17 Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana.
18 Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.