Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 15:5-41 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 15:5-41 in Biblia Takatifu

5 Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, “Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata Sheria ya Mose.”
6 Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa kuchunguza jambo hilo.
7 Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, “Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia na kuamini.
8 Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.
9 Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.
10 Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?
11 Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.”
12 Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.
13 Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: “Ndugu zangu, nisikilizeni!
14 Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.
15 Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
16 Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena.
17 Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana.
18 Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.
19 “Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: tusiwataabishe watu wa mataifa wanomgeukia Mungu.
20 Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa najisi kwa kutambikiwa sanamu za miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu.
21 Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato.”
22 Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu.
23 Wakawapa barua hii: “Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, tunawasalimuni ninyi ndugu wa mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia.
24 Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu.
25 Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo,
26 ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
27 Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika.
28 Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike mzigo zaidi ya mambo haya muhimu:
29 Msile vyakula vilivyotambikiwa sanamu; msinywe damu; msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!”
30 Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua.
31 Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo, wakafurahi sana.
32 Yuda na Sila, ambao nao walikuwa manabii, walizungumza na hao ndugu kwa muda mrefu wakiwatia moyo na kuwaimarisha.
33 Baada ya kukaa huko kwa muda fulani, ndugu wa Antiokia waliwaaga wakiwatakia amani, kisha wakarudi kwa wale waliokuwa wamewatuma.
34 Lakini Sila aliamua kubaki.
35 Paulo na Barnaba walibaki huko Antiokia kwa muda; wakafundisha na kuhubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.
36 Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la Bwana tukajionee jinsi wanavyoendelea.”
37 Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko.
38 Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao.
39 Basi kukatokea ubishi mkali kati yao, na wakaachana. Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro.
40 Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka.
41 Katika safari hiyo alipitia Siria na Kilikia akiyaimarisha makanisa.
Matendo 15 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 15:5-41 in Biblia ya Kiswahili

5 Lakini watu fulani walioamini, waliokuwa katika kundi la Mafarisayo, walisimama nakusema, “ni muhimu kuwatahiri na kuwaamuru waishike sheria ya Musa.”
6 Hivyo mitume na wazee walisimama pamoja kulifikiria hili swala.
7 Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama na kusema kwao, “Ndugu mwatambua kwamba kitambo kizuri kilichopita Mungu alifanya chaguo kati yenu, kwamba kwa mdomo wangu Mataifa wasikie neno la injili, na kuamini.
8 Mungu, anayefahamu mioyo, anashuhudia kwao, anawapa Roho mtakatifu, kama alivyofanya kwetu;
9 na hakutengeneza utofauti kati yetu na wao, akiifanya mioyo yao safi kwa imani.
10 Kwa hiyo, kwa nini mnamjaribu Mungu kwamba muweke nira juu ya shingo za wanafunzi ambayo hata baba zetu wala sisi hatukuweza kustahimili?
11 Lakini twaamini kwamba tutaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu, kama walivyokuwa.”
12 Kusanyiko lote lilinyamaza walipokua wakimsikiliza Barnaba na Paulo walipokuwa wakitoa taarifa ya ishara na maajabu ambayo Mungu alifanya pamoja nao kati ya watu wa mataifa.
13 Walipoacha kuongea, Yakobo alijibu akisema, “Ndugu nisikilizeni.
14 Simoni ameelezea jinsi kwanza Mungu kwa neema aliwasaidia Mataifa ili kwamba ajipatie kutoka kwao watu kwa ajili ya jina lake.
15 Maneno ya manabii yanakubaliana na hili kama lilivyoandikwa.
16 'Baada ya mambo haya nitarudi na kuijenga tena hema ya Daudi, iliyoanguka chini; nitainua na kuhuisha uhararibifu wake,
17 ili kwamba watu waliobaki wamtafute Bwana, pamoja na watu wa Mataifa walioitwa kwa jina langu.'
18 Hivi ndivyo asemavyo Bwana aliyefanya mambo haya yajulikanayo tangu enzi za zamani.
19 Hivyo basi, ushauri wangu ni, kwamba tusiwapatie shida watu wa Mataifa wamgeukiao Mungu;
20 lakini tuandike kwao kwamba wajiepushe mbali na uharibifu wa sanamu, tamaa za uasherati, na vilivyonyongwa, na damu.
21 Kutoka vizazi vya wazee kuna watu katika kila mji wahubirio na kumsoma Musa katika masinagogi kila Sabato.”
22 Kwa hiyo ikaonekana kuwa imewapendeza mitume na wazee, pamoja na kanisa lote, kumchagua Yuda aliyeitwa Barsaba, na Silas, waliokuwa viongozi wa kanisa, na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba.
23 Waliandika hivi, “Mitume, wazee na ndugu, kwa ndugu wa Mataifa walioko Antiokia, Shamu na Kilikia, salamu.
24 Tulisika kwamba watu fulani ambao hatukuwapatia amri hiyo, walitoka kwetu na wamewataabisha kwa mafundisho yaletayo shida nafsini mwenu.
25 Kwa hiyo imeonekana vyema kwetu sote kuchagua watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,
26 watu walio hatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana Yesu Kristo.
27 Kwa hiyo tumemtuma Yuda na Sila, watawaambia mambo yayo hayo.
28 Kwa kuwa ilionekana vyema kwa Roho Mtakatifu na kwetu, kutoweka juu yenu mzigo mkubwa kuliko mambo haya yaliyo ya lazima:
29 kwamba mgeuke kutoka kwenye vitu vitolewavyo kwa sanamu, damu, vitu vya kunyongwa, na uasherati. Kama mtajiweka mbali na hivi, itakuwa vyema kwenu. Kwa herini.”
30 Hivyo basi, walivyotawanyishwa, waliteremkia Antiokia; baada ya kukusanya kusanyiko pamoja, waliwasilisha barua.
31 Walipokua wameisoma, walifurahi kwa sababu ya kutiwa moyo.
32 Yuda na Sila, na manabii, waliwatia moyo ndugu kwa maneno mengi na kuwatia nguvu.
33 Baada ya kukaa muda fulani huko, walitawanyishwa kwa amani kutoka kwa ndugu kwa wale waliowatuma.
34 Lakini ilionekana vyema Sila kubaki huko
35 Lakini Paulo na wengine walikaa Antiokia pamoja na wengine wengi, ambapo walifundisha na kuhubiri neno la Bwana.
36 Baada ya siku kadhaa Paulo alisema kwa Barnaba, “Na turudi sasa na kuwatembelea ndugu katika kila mji tulipohubiri neno la Bwana, na kuwaona walivyo.
37 Barnaba alihitaji pia kumchukua pamoja nao Yohana aliyeitwa Marko.
38 Lakini Paulo alifikiria haikuwa vizuri kumchukua Marko, aliyewaacha huko Pamfilia na hakuendelea nao katika kazi.
39 Kisha hapo kukatokea mabishano makubwa kwa hiyo walitengana, na Barnaba alimchukua Marko na kusafiri kwa meli mpaka Kipro,
40 Lakini Paulo alimchagua Sila na kuondoka, baada ya kukabidhiwa na ndugu katika neema ya Bwana.
41 Na alienda kupitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa.
Matendo ya Mitume 15 in Biblia ya Kiswahili