26 “Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.
27 Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi. Wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo.
28 Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe.
29 Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini.
30 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu.
31 Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli.
32 Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu.
33 Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili: Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.
34 Na juu ya kumfufua kutoka wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.
35 Naam, na katika sehemu nyingine za zaburi asema: Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.
36 Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza mapenzi ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza.
37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza.
38 Jueni wazi, ndugu zangu, kwamba ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu kwa njia ya Yesu Kristo;
39 na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya Sheria ya Mose.
40 Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii:
41 Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni.”
42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika ile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo.
43 Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu.
44 Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana.
45 Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana.
46 Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, “Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni ninyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uzima wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine.
47 Maana Bwana alituagiza hivi: Nimekuteua wewe uwe mwanga kwa mataifa, uwe njia ya wokovu kwa ulimwengu wote.”
48 Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uzima wa milele, wakawa waumini.