3 Hapo zikawatokea ndimi, kama ndimi za moto zimegawanyika, zikawa juu yao kila mmoja wao.
4 Wao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu na wakaanza kusema kwa lugha zingine, kama vile Roho alivyowajalia kusema.
5 Sasa walikuwapo wayahudi waliokuwa wanaishi Yerusalemu, wacha Mungu, kutoka kila taifa chini ya mbingu.
6 Ngurumo hizi ziliposikiwa, kundi la watu likaja pamoja na wakiwa na wasiwasi kwa sababu kila mtu aliwasikia wakiongea kwa lugha yake mwenyewe.
7 waliduwaa na kushangazwa, wao walisema, “Kweli, hawa wote wanaoongea siyo Wagalilaya?
8 Kwa nini sisi tunawasikia, kila mmoja katika lugha tulizozaliwa nazo?
9 Waparthia na Wamedi na Waelamu, na hao waishio Mesopotamia, Uyahudi, na Kapadokia, na katika Ponto na Asia,
10 katika Frigia, Pamfilia, katika Misri, na sehemu ya Libya hata Kirene, na wageni kutoka Rumi,
11 Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, tunawasikia wakizungumza katika lugha zetu kuhusu kazi za uweza wa Mungu.”
12 Wote walikuwa wameduwaa na kutatanishwa; walisemezana wao kwa wao, “Hii ina maana gani?”
13 Lakini wengine walidhihaki wakisema, “Hawa wamejazwa kwa mvinyo mpya.”
14 Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti, akawaambia, “Watu wa Yudea na wote mnaoishi hapa Yerusalemu, hili lijulikane kwenu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.
15 Watu hawa hawajalewa kama mnavyodhani, sababu saa hizi ni asubuhi saa tatu.
16 Lakini hili lilikuwa limesemwa kupitia kwa nabii Yoeli:
17 Itakuwa katika siku za mwisho; Mungu asema, nitamwaga Roho wangu kwa watu wote. Wana wenu na binti zenu watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
18 Vilevile juu ya watumishi wangu na watumishi wangu wa kike katika siku hizo, nitamwaga Roho wangu, nao watatabiri.
19 Nitaonesha maajabu juu angani na ishara chini duniani, damu, moto, na mafusho ya moshi.
20 Na jua litabadilishwa kuwa giza na mwezi kuwa damu, kabla haijaja siku kuu na ya ajabu ya Bwana.
21 itakuwa ya kwamba kila mmoja ambaye huliitia jina la Bwana ataokoka.'
22 Watu wa Israeli, sikieni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mwanadamu aliyethibitishwa na Mungu kwenu kwa matendo ya uweza na maajabu, na ishara ambazo Mungu kupitia Yeye katikati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua-
23 Kwa sababu ya mpango uliokusudiwa tangu mwanzo, na maarifa ya Mungu, alitolewa, na ninyi, kwa mikono ya watu wahalifu, mlimsulibisha na kumuua,
24 ambaye Mungu alimwinua, akauondoa uchungu wa mauti kwake, kwasababu haikuwezekana kwake kumilikiwa na huo.