Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 21:2-33 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 21:2-33 in Biblia Takatifu

2 Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri.
3 Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake.
4 Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa waongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.
5 Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali.
6 Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli nao wakarudi makwao.
7 Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja.
8 Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko Kaisarea tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu.
9 Alikuwa na binti watatu ambao walikuwa na kipaji cha unabii.
10 Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea.
11 Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema “Roho Mtakatifu asema hivi: Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye ukanda na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa.”
12 Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu.
13 Lakini yeye alijibu, “Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu.”
14 Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: “Mapenzi ya Bwana yafanyike”
15 Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu.
16 Wengine kati ya wale wafuasi wa Kaisarea walienda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa muumini kwa siku nyingi.
17 Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana.
18 Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwako pia.
19 Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya mataifa kwa njia ya utumishi wake.
20 Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanashika kwa makini Sheria ya Mose.
21 Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa mengine kuwa wasiijali Sheria ya Mose, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi.
22 Sasa, mambo yatakuwaje? Ni dhahiri kuwa watapata habari kwamba umekwisha wasili hapa.
23 Basi, fanya kama tunavyokushauri. Tunao hapa watu wanne ambao wameweka nadhiri.
24 Jiunge nao katika ibada ya kujitakasa, ukalipe na gharama zinazohusika, kisha wanyolewe nywele zao. Hivyo watu wote watatambua kwamba habari zile walizoambiwa juu yako hazina msingi wowote, na kwamba wewe binafsi bado unaishi kufuatana na maagizo ya Sheria za Mose.
25 Kuhusu wale watu wa mataifa mengine ambao wamekuwa waumini, tumekwisha wapelekea barua tukiwaambia mambo tuliyoamua: wasile chochote kilichotambikiwa miungu ya uongo, wasinywe damu, wasile nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
26 Basi, kesho yake Paulo aliwachukua wale watu akafanya ibada ya kujitakasa pamoja nao. Kisha akaingia Hekaluni kutoa taarifa kuhusu mwisho wa siku za kujitakasa na kuhusu dhabihu itakayotolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
27 Wakati siku hizo saba zilipokaribia kuisha, Wayahudi waliokuwa wametoka katika mkoa wa Asia walimwona Paulo Hekaluni. Wakachochea hasira kati ya kundi lote la watu, wakamtia nguvuni
28 wakipiga kelele: “Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga Sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine Hekaluni na kupatia najisi mahali hapa patakatifu.”
29 Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo mwenyeji, wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.
30 Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya Hekalu na papo hapo milango ya Hekalu ikafungwa.
31 Walikuwa tayari kumuua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.
32 Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.
33 Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, “Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?”
Matendo 21 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 21:2-33 in Biblia ya Kiswahili

2 Tulipopata meli inayovuka kwenda Foinike, tulipanda tukasafiri.
3 Tulipofika mbele ya kisiwa cha Kipro, tukaiacha upande wa kushoto, tukasafiri hadi Siria, tukaweka nanga katika mji wa Tiro, kwa sababu huko ndiko meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake.
4 Baada ya kuwaona wanafunzi, tukakaa huko siku saba. Wanafunzi hawa wakamwambia Paulo kupitia kwa Roho kwamba yeye asikanyage Yerusalemu.
5 Hata tulipotimiza siku zile, sisi tukaondoka tukaenda zetu. Wote pamoja, na wanawake zao na watoto wao, walitusindikiza katika njia zetu hadi tulipotoka nje ya mji. Kisha tukapiga magoti pwani, tukaomba, tukaagana kila mmoja.
6 Tukapanda meli, huku nao wakarudi nyumbani kwao tena.
7 Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro, tukafika Tolemai. Pale tulisalimia ndugu, na kukakaa nao kwa siku moja.
8 Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisaria. Sisi tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, nasi tukakaa pamoja naye.
9 Mtu huyu alikuwa na mabinti wanne mabikira ambao walitabiri.
10 Baada ya kukaa huko kwa siku kadhaa, akashuka kutoka Uyahudi nabii mmoja aitwaye Agabo.
11 Yeye alikuja kwetu na akautwaa mkanda wa Paulo. kwa huo alijifunga miguu na mikono yake mwenyewe na kusema, “Roho Mtakatifu asema hivi,” “Wayahudi wa Yerusalemu watamfunga mtu anayemiliki mkanda huu, nao watamkabidhi mikononi mwa watu wa mataifa.”
12 Tuliposikia mambo hayo, sisi na watu waliokuwa wakiishi mahali pale tulimsihi Paulo asipande kwende Yerusalemu.
13 Ndipo Paulo alijibu, “Mnafanya nini, mnalia na kunivunja moyo wangu? Kwa maana niko tayari, siyo tu kufungwa, lakini pia kufia huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”
14 Kwa vile Paulo hakutaka kushawishiwa, tuliacha na kusema, “Basi mapenzi ya Bwana yafanyike.”
15 Baada ya siku hizi, tulichukua mifuko yetu na tukapanda Yerusalemu.
16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria pia walifuatana nasi. Wakamleta mtu mmoja aitwaye Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani, ambaye tulikaa naye.
17 Tulipofika Yerusalemu, ndugu walitukaribisha kwa furaha.
18 Kesho yake Paulo alienda pamoja nasi kwa Yakobo, na wazee wote walikuwepo.
19 Baada ya kuwasalimu, aliwapa taarifa moja baada ya nyingine ya mambo ambayo Mungu aliyotenda miongoni mwa mataifa kwa kupitia huduma yake.
20 Wakati waliposikia hayo, wakamsifu Mungu, na wakamwambia, “Unaona, ndugu, kuna maelfu wangapi wameamini miongoni mwa Wayahudi. Wao wote wana nia ya kushika sheria.
21 Wameambiwa kuhusu wewe, kwamba unafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa kuachana na Musa, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao, na wasifuate desturi za zamani.
22 Tunapaswa tufanye nini? Bila shaka watasikia kwamba wewe umekuja.
23 Hivyo fanya kile sisi tunachokuambia sasa: tunao watu wanne ambao wameweka nadhiri.
24 Wachukue watu hawa na ujitakase mwenyewe pamoja nao, na uwalipie gharama zao, ili waweze kunyoa vichwa vyao. Hivyo kila mmoja apate kujua kwamba mambo waliyoambiwa kuhusu wewe ni ya uongo. Watajifunza kwamba wewe pia unafuata sheria.
25 Lakini kwa habari za mataifa ambao wamekuwa waumini, tuliandika na kutoa maagizo kwamba wanapaswa kujiepusha na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu, na damu, kutokana na kile kilichonyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
26 Ndipo, Paulo aliwatwaa wanaume, na siku ya pili, akajitakasa mwenyewe pamoja nao, akaingia Hekaluni, kutangaza kipindi cha siku za kujitakasa, hadi sadaka itolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
27 Siku hizo saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka Asia wakamuona Paulo Hekaluni, na makutano wakakasirika, na wakamnyoshea mikono.
28 Walikuwa wanapiga kelele, “Watu wa Israeli, tusaidieni. Huyu ni yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo ambayo ni kinyume na watu, sheria, na mahali hapa. Pia amewaleta Wayunani katika Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”
29 Kwa kuwa mwanzoni walikuwa wamemwona Trofimo Muefeso akiwa pamoja naye mjini, nao walidhani kwamba Paulo alimleta hekaluni.
30 Mji wote ulikuwa na taharuki, na watu wakakimbia pamoja na kumkamata Paulo. Wakamtoa nje ya Hekalu, na milango mara ikafungwa.
31 Walipokuwa wakijaribu kumuua, habari zilimfikia mkuu wa jeshi la walinzi kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.
32 Mara hiyo akawachukua askari na jemadari akaukimbilia umati. Wakati Watu walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.
33 Kisha mkuu wa jeshi alimkaribia na akamshika Paulo, na akaamuru afungwe minyororo miwili. Akamuuliza yeye ni nani na amefanya nini.
Matendo ya Mitume 21 in Biblia ya Kiswahili