Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 20:18-38 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 20:18-38 in Biblia Takatifu

18 Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyotumia wakati wote pamoja nanyi tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia.
19 Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi.
20 Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni.
21 Niliwaonya wote—Wayahudi kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu.
22 Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko.
23 Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea.
24 Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa ni kitu sana kwangu. Nataka tu nikamilishe ule utume wangu na kumaliza ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nitangaze Habari Njema ya neema ya Mungu.
25 “Nimekuwa nikienda huko na huko kati yenu nikiuhubiri Ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena.
26 Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote.
27 Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu.
28 Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae.
29 Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo.
30 Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu.
31 Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi.
32 “Na sasa basi, ninawaweka ninyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga ninyi na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake.
33 Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote.
34 Mnajua ninyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu.
35 Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: Heri zaidi kutoa kuliko kupokea.”
36 Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali.
37 Wote walikuwa wanalia; wakamwaga kwa kumkumbatia na kumbusu.
38 Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini.
Matendo 20 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 20:18-38 in Biblia ya Kiswahili

18 Walipofika kwake, akawaambia, ninyi wenyewe mwajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu muda wote.
19 Nimemtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi, na mateso yaliyonipata mimi kwa hila za Wayahudi.
20 Mwajua jinsi ambavyo sikujizuia kutangaza kwenu kitu chochote ambacho kilikuwa muhimu, na jinsi mimi nilivyowafundisha wazi wazi na pia kwenda nyumba kwa nyumba.
21 Mnajua jinsi mimi nilivyoendelea kuwaonya Wayahudi na Wayunani juu ya toba kwa Mungu na imani katika Bwana wetu Yesu.
22 Na sasa, angalieni, mimi, nikiwa ninamtii Roho Mtakatifu kuelekea Yerusalemu, nisiyajue mambo ambayo yatanitokea mimi huko,
23 ila kwa kuwa Roho Mtakatifu hunishuhudia mimi katika kila mji na anasema kwamba minyororo na mateso ndivyo vinavyoningojea.
24 Lakini mimi si kufikiria kwamba maisha yangu ni kwa njia yoyote ya thamani kwangu, ili niweze kumaliza mwendo wangu na huduma niliyopokea kutoka kwa Bwana Yesu, kuishuhudia injili ya neema ya Mungu.
25 Na sasa, tazama, najua kwamba wote, miongoni mwa wale nilioenda kuwahubiri Ufalme, hamtaniona uso tena.
26 Kwa hiyo nawashuhudia leo hii, kwamba sina hatia kwa damu ya mtu yeyote.
27 Kwa maana sikujizuia kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.
28 Kwa hiyo iweni waangalifu juu yenu ninyi wenyewe, na juu ya kundi lolote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi. Iweni waangalifu kulichunga kusanyiko la Bwana, ambalo alilinunua kwa damu yake mwenyewe.
29 Najua kwamba baada ya kuondoka kwangu, mbwa mwitu wakali wataingia kwenu, na wasilihurumie kundi.
30 Najua kwamba hata miongoni mwenu wenyewe baadhi ya watu watakuja na kusema mambo mapotovu, ili kuwavuta wanafunzi wawafuate wao.
31 Kwa hiyo muwe macho. Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuweza kuacha kuwafundisha kila mmoja wenu kwa machozi usiku na mchana.
32 Na sasa mimi nawakabidhi kwa Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliowekwa wakfu kwa Mungu.
33 Sikutamani fedha, dhahabu, au mavazi.
34 Mnajua ninyi wenyewe kwamba mikono hii imenipatia mahitaji yangu mwenyewe na mahitaji ya wale waliokuwa pamoja nami.
35 Katika mambo yote niliwapa mfano wa jinsi inavyopasa kuwasaidia wanyonge kwa kufanya kazi, na jinsi mnavyopaswa kukumbuka maneno ya Bwana Yesu, maneno ambayo yeye mwenyewe alisema: “Ni heri kutoa kuliko kupokea.”
36 Baada ya kusema namna hii, alipiga magoti akaomba pamoja nao.
37 Wote wakalia sana na kumwangukia Paulo shingoni na kumbusu.
38 Walihuzunika zaidi ya yote kwa sababu ya kile ambacho alikuwa amesema, kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Kisha wakamsindikiza merikebuni.
Matendo ya Mitume 20 in Biblia ya Kiswahili