Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Marko 6:31-46 in Swahili (individual language)

Help us?

Marko 6:31-46 in Biblia Takatifu

31 Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno walikuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. Basi, Yesu akawaambia, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha kula chakula, mkapumzike kidogo.”
32 Basi, Wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha.
33 Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika.
34 Waliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, “Hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa.
36 Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula.”
37 Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni ninyi chakula.” Nao wakamwuliza, “Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari mia mbili, na kuwapa chakula?”
38 Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame.” Walipokwisha tazama, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”
39 Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi.
40 Nao wakaketi makundimakundi ya watu mia moja na ya watu hamsini.
41 Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote.
42 Watu wote wakala, wakashiba.
43 Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili.
44 Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume elfu tano.
45 Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ng'ambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu.
46 Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali.
Marko 6 in Biblia Takatifu

Marko 6:31-46 in Biblia ya Kiswahili

31 Naye akawaambia, “Njooni wenyewe mahali pa faragha na tupumzike kwa muda.” Watu wengi walikuwa wanakuja na kuondoka, hata hawakupata nafasi ya kula.
32 Hivyo wakapanda mashua wakaenda mahali pa faragha peke yao.
33 Lakini waliwaona wakiondoka na wengi wakawatambua, kwa pamoja walikimbia kwa miguu kutoka miji yote, nao wakafika kabla yao.
34 Walipofika pwani, aliona umati mkubwa na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Na akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Muda ulipoendelea sana, wanafunzi wakamjia wakamwambia, “Hapa ni mahali pa faragha na muda umeendelea.
36 Uwaage waende miji ya jirani na vijiji ili wakajinunulie chakula.”
37 Lakini akawajibu akisema, “Wapeni ninyi chakula.” Wakamwambia, “Tunaweza kwenda na kununua mikate yenye thamani ya dinari mia mbili na kuwapa wale?”
38 Akawambia,” Mna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.” walipopata wakamwambia, “Mikate mitano na samaki wawili.”
39 Akawaamuru watu waketi katika makundi juu ya majani mabichi.
40 Wakawaketisha katika makundi; makundi ya mamia kwa hamsini.
41 Kisha akachukua mikate mitano na samaki wawili, na kutazama mbinguni, akaibariki kisha akawapa wanafunzi waweke mbele ya umati. Na kisha aligawa samaki wawili kwa watu wote.
42 Walikula wote hadi wakatosheka.
43 Walikusanya vipande vya mikate iliyobaki, Vikajaa vikapu kumi na viwili, na pia vipande vya samaki.
44 Na walikuwa wanaume elfu tano waliokula mikate.
45 Mara akawaambia wapande kwenye mashua waende sehemu nyingine, hadi Bethsaida, wakati Yeye akiwaaga makutano.
46 Walipokuwa wamekwisha kuondoka, akaenda mlimani kuomba.
Marko 6 in Biblia ya Kiswahili