Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Luka 2:9-40 in Swahili (individual language)

Help us?

Luka 2:9-40 in Biblia Takatifu

9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.
10 Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote.
11 Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.
12 Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.”
13 Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:
14 “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!”
15 Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.”
16 Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.
17 Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.
18 Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.
19 Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.
20 Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.
21 Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
22 Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana.
23 Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.”
24 Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana.
25 Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.
26 Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana.
27 Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria,
28 Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema:
29 “Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
30 Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako,
31 ambao umeutayarisha mbele ya watu wote:
32 Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli.”
33 Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto.
34 Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu;
35 na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.”
36 Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa.
37 Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana.
38 Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.
39 Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya.
40 Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye.
Luka 2 in Biblia Takatifu

Luka 2:9-40 in Biblia ya Kiswahili

9 Ghafla, malaika wa Bwana akawatokea, na utukufu wa Bwana ukang'aa kuwazunguka, na wakawa na hofu sana.
10 Ndipo malaika akwaambia, “Msiogope, kwasababu nawaletea habari njema ambayo italeta furaha kuu kwa watu wote.
11 Leo Mwokozi kazaliwa kwaajili yenu mjini mwa Daudi! Yeye ndiye Kristo Bwana!
12 Hii ndiyo ishara ambayo mtapewa, mtamkuta mtoto amefungwa nguo na amelala kwenye hori la kulishia wanyama.”
13 Ghafla kukawa na jeshi kubwa la mbinguni likaungana na malaika huyo wakamsifu Mungu, wakisema,
14 “Utukufu kwa Mungu aliye juu sana, na amani iwe duniani kwa wote ambao anapendezwa nao.”
15 Ikawa kwamba malaika walipokwisha kuondoka kwenda mbinguni, wachungaji wakasemezena wao kwa wao, “Twendeni sasa kule Bethlehemu, na tukaone hiki kitu ambacho kimetokea, ambacho Bwana ametufahamisha.”
16 Wakaharakisha kule, na wakamkuta Mariamu na Yusufu, na wakamuona mtoto amelala kwenye hori la kulishia wanyama.
17 Na walipoona hivi, wakawajulisha watu kile walichokuwa wameambiwa kumhusu mtoto.
18 Wote waliosikia habari hii wakashangazwa na kile kilichosemwa na wachungaji.
19 Lakini Mariamu akaendelea kufikiri kuhusu yote aliyokwisha kuyasikia, akiyatunza moyoni mwake.
20 Wachungaji wakarudi wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa ajili ya kila kitu walichokwisha sikia na kuona, kama tu ilivyokuwa imenenwa kwao.
21 Ilipofika siku ya nane na ilikuwa ni wakati wa kumtahiri mtoto, wakamwita jina Yesu, jina alilokwishapewa na yule malaika kabla mimba haijatungwa tumboni.
22 zao zilizotakiwa za utakaso zilipopita, kulingana na sheria ya Musa, Yusufu na Mariamu wakampeleka hekaluni kule Yerusalemu kumweka mbele za Bwana.
23 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, “Kila mwanaume anayefungua tumbo ataitwa aliyetolewa wakfu kwa Bwana.”
24 Wao vilevile walikuja kutoa sadaka kulingana na kile kinachosemwa katika sheria ya Bwana, “Jozi ya njiwa au makinda mawili ya njiwa.”
25 Tazama, palikuwa na mtu katika Yerusalemu ambaye jina lake alikuwa akiitwa Simeoni. mtu huyu alikuwa mwenye haki na mcha Mungu. Yeye alikuwa akisubiri kwa ajili ya mfariji wa Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.
26 Ilikuwa imekwisha funuliwa kwake kupitia Roho Mtakatifu kwamba yeye hangelikufa kabla ya kuwomwona Kristo wa Bwana.
27 Siku moja alikuja ndani ya hekalu, akiongozwa na Roho Mtakatifu. Ambapo wazazi walimleta mtoto, Yesu, kumfanyia yale yaliyopasa kawaida ya sheria,
28 ndipo Simeoni alimpokea mikononi mwake, na akamsifu Mungu na kusema,
29 “Sasa ruhusu mtumishi wako aende kwa amani Bwana, kulingana na Neno lako.
30 Kwa kuwa macho yangu yameuona wakovu wako,
31 ambao umeonekana kwa macho ya watu wote.
32 Yeye ni nuru kwa ajili ya ufunuo kwa Wamataifa na utukufu wa watu Israeli.”
33 Baba na Mama wa mtoto walishangazwa kwa mambo ambayo yalizungumzwa juu yake.
34 Ndipo Simeoni akawabariki na akasema kwa Mariamu mama yake, “Sikiliza kwa makini! Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli na ni ishara ambayo watu wengi wataipinga.
35 Pia ni upanga utakaochoma nafsi yako mwenyewe, ili kwamba mawazo ya mioyo ya wengi yadhihirike”.
36 Nabii mwanamke aliyeitwa Ana pia alikuwako hekaluni. Yeye alikuwa binti wa Fanueli kutoka kabila la Asheri. Alikuwa na miaka mingi sana. Naye aliishi na mume wake kwa miaka saba baada ya kuoana,
37 na ndipo akawa mjane kwa miaka themanini na minne. Naye hakuwahi kuondoka hekaluni na alikuwa akiendelea kumwabudu Mungu pamoja na kufunga na kuomba, usiku na mchana.
38 Na kwa wakati huo, alikuja pale walipo akaanza kumshukuru Mungu. Aliongea kumhusu mtoto kwa kila mtu ambaye alikuwa akisubiri ukombozi wa Yerusalemu.
39 Walipomaliza kila kitu walichotakiwa kufanya kuligana na na sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, mjini kwao, Nazareti.
40 Mtoto alikua, na akawa na nguvu, akiongezeka katika hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Luka 2 in Biblia ya Kiswahili