Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Luka 23:2-25 in Swahili (individual language)

Help us?

Luka 23:2-25 in Biblia Takatifu

2 Wakaanza kumshtaki wakisema: “Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme.”
3 Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.”
4 Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, “Sioni kosa lolote katika mtu huyu.”
5 Lakini wao wakasisitiza wakisema: “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa.”
6 Pilato aliposikia hayo, akauliza, “Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?”
7 Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu.
8 Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza.
9 Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno.
10 Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
11 Basi, herode pamoja na maaskari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato.
12 Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki.
13 Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu,
14 akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake.
15 Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo.
16 Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.”
17 Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!”
19 (Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)
20 Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;
21 lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!”
22 Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya kosa gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”
23 Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.
24 Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.
25 Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
Luka 23 in Biblia Takatifu

Luka 23:2-25 in Biblia ya Kiswahili

2 Wakaanza kumshutumu, wakisema, “Tumemkuta mtu huyu akipotosha taifa letu, kwa kukataza tusitoe kodi kwa Kaisari, na akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, Mfalme.”
3 Pilato akamuuliza, akisema, “Je wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Na Yesu akamjibu akisema, “Wewe wasema hivyo”.
4 Pilato akamuambia kuhani mkuu na makutano, “Sioni kosa kwa mtu huyu”.
5 Lakini wao wakasisitiza, wakisema, “Amekuwa akiwachochea watu, akifundisha katika Uyahudi yote, kuanzia Galilaya na sasa yuko hapa.”
6 Pilato aliposikia haya, akaulizia kama mtu huyo ni wa Galilaya?
7 Alipotambua kuwa alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka Yesu kwa Herode, ambaye naye alikuwa Yerusalemu kwa siku hizo.
8 Herode alipomuona Yesu, alifurahi sana kwasababu alitaka kumuona kwa siku nyingi. Alisikia habari zake na alitamani kuona moja ya miujiza ikifanywa na yeye.
9 Herode alimhoji Yesu kwa maneno mengi, lakini Yesu hakumjibu chochote.
10 Makuhani wakuu pamoja na waandishi walisimama kwa ukali wakimshitaki.
11 Herode pamoja na maaskari wake, walimtukana na kumdhihaki, na kumvika mavazi mazuri, kisha akamrudisha Yesu kwa Pilato.
12 Herode na Pilato wakawa marafiki kuanzia siku hiyo, (kabla ya hapo walikuwa maadui).
13 Pilato akawaita pomoja makuhani wakuu na watawala na umati wa watu,
14 Akawaambia, “Mmeniletea mtu huyu kama mtu anaye waongoza watu wafanye mabaya, na tazama, baada ya kuwa nimemhoji mbele yenu, sikuona kosa kwa mtu huyu kuhusu mambo yote ambayo ninyi mnamshitaki yeye.
15 Hapana, wala Herode, kwa maana amemrudisha kwetu, na tazama hakuna chochote alichokifanya kinachostahili adhabu ya kifo.
16 Kwahiyo basi nitamuadhibu na kumuachilia.
17 (Sasa, Pilato anawajibika kumuachilia mfungwa mmoja kwa wayahudi wakati wa sikukuu).
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja, wakisema, “Mwondoe huyo, na tufungulie Baraba!”
19 Baraba alikuwa ni mtu ambaye amewekwa gerezani kwa sababu ya uasi fulani katika jiji na kwa kuua.
20 Pilato akawaambia tena, akitamani kumwachilia Yesu.
21 Lakini wao wakapiga kelele, wakisema, “Msulibishe, msulibishe.”
22 Akawauliza kwa mara ya tatu, “kwa nini, huyu mtu amefanya maovu gani? Sikupata kosa linalostahili adhabu ya kifo kwake. Kwahiyo nitakapo maliza kumuadhibu nitamuachilia.”
23 Lakini wakasisitiza kwa sauti ya juu, wakitaka asulubiwe. Na sauti zao zikamshawishi Pilato.
24 Hivyo Pilato akaamua kuwapatia matakwa yao.
25 Akamuachilia yule waliyemtaka ambaye alifungwa kwa kusababisha ghasia na kuua. Lakini akamtoa Yesu kwa matakwa yao.
Luka 23 in Biblia ya Kiswahili