Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Luka 23:17-53 in Swahili (individual language)

Help us?

Luka 23:17-53 in Biblia Takatifu

17 Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!”
19 (Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)
20 Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;
21 lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!”
22 Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya kosa gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”
23 Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.
24 Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.
25 Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
26 Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu.
27 Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia.
28 Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu.
29 Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!
30 Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: Tuangukieni! na vilima, Tufunikeni!
31 Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?”
32 Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.
34 Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
35 Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!”
36 Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki
37 wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
38 Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.”
39 Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.”
40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.
41 Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”
42 Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.”
43 Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.”
44 Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likafunika nchi yote mpaka saa tisa,
45 na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka vipande viwili.
46 Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, naiweka roho yangu mikononi mwako.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.
47 Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.”
48 Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni.
49 Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
50 Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Armathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika;
51 Alikuwa akitazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao.
52 Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
53 Kisha, akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika.
Luka 23 in Biblia Takatifu

Luka 23:17-53 in Biblia ya Kiswahili

17 (Sasa, Pilato anawajibika kumuachilia mfungwa mmoja kwa wayahudi wakati wa sikukuu).
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja, wakisema, “Mwondoe huyo, na tufungulie Baraba!”
19 Baraba alikuwa ni mtu ambaye amewekwa gerezani kwa sababu ya uasi fulani katika jiji na kwa kuua.
20 Pilato akawaambia tena, akitamani kumwachilia Yesu.
21 Lakini wao wakapiga kelele, wakisema, “Msulibishe, msulibishe.”
22 Akawauliza kwa mara ya tatu, “kwa nini, huyu mtu amefanya maovu gani? Sikupata kosa linalostahili adhabu ya kifo kwake. Kwahiyo nitakapo maliza kumuadhibu nitamuachilia.”
23 Lakini wakasisitiza kwa sauti ya juu, wakitaka asulubiwe. Na sauti zao zikamshawishi Pilato.
24 Hivyo Pilato akaamua kuwapatia matakwa yao.
25 Akamuachilia yule waliyemtaka ambaye alifungwa kwa kusababisha ghasia na kuua. Lakini akamtoa Yesu kwa matakwa yao.
26 Walipokuwa wakimpeleka, walimkamata mtu mmoja aitwaye Simoni wa Ukirene, akitokea katika nchi, wakamtwika msalaba ili abebe, akimfuata Yesu.
27 umati mkubwa wa watu, na wanawake ambao walihuzunika na kuomboleza kwa ajili yake, walikuwa wakimfuata.
28 Lakini akawageukia, Yesu akawaambia, 'Mabinti wa Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni ninyi wenyewe na kwa ya ajili watoto wenu.
29 Tazama, siku zinakuja ambazo watasema, “Wamebarikiwa walio tasa na matumbo yasiyozaa, na matiti ambayo hayakunyonyesha.
30 Ndipo watakapo anza kuiambia milima, 'Tuangukieni,' na vilima, 'Mtufunike.'
31 Maana kama wakifanya mambo haya ikiwa mti mbichi, itakuwaje ukiwa mkavu?”
32 wanaume wengine, wahalifu wawili, walipelekwa pamoja naye ili wauwawe.
33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la kichwa, ndipo wakamsulubisha pamoja na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto.
34 Yesu alisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. “Nao wakapiga kura, kugawa mavazi yake.
35 Watu walikuwa wamesimama wakiangalia huku watawala wakimdhihaki, wakisema, “Aliwaokoa wengine. Sasa ajiokoe mwenyewe, kama yeye ni Kristo wa Mungu, mteule”.
36 Askari pia walimdharau, walimkaribia yeye na wakumpa siki,
37 wakisema, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi jiokoe mwenyewe”
38 Kulikuwa pia na alama juu yake iliyoandikwa “HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.”
39 Mmoja wa wahalifu aliyesulubishwa alimtukana akisema, “Wewe si Kristo? jiokoe mwenyewe na sisi”
40 Lakini yule mwingine akajibu, akimkemea na akisema, “Je wewe humuogopi Mungu, nawe uko katika hukumu hiyo hiyo?
41 Sisi tupo hapa kwa haki, kwa maana sisi tunapokea kile tunachostahili kwa matendo yetu. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”
42 Na aliongeza, “Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”
43 Yesu akamwambia, “Amini nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
44 Hapo ilikuwa karibu saa ya sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa ya tisa,
45 Mwanga wa jua ulizimika. Kisha pazia la hekalu likagawanyika katikati kuanzia juu.
46 Akilia kwa sauti kuu, Yesu alisema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu,” baada ya kusema haya, akafa.
47 Wakati Akida alipoona yaliyotendeka alimtukuza Mungu akisema, “Hakika huyu alikuwa mtu mwenye haki.”
48 Wakati umati wa watu waliokuja pamoja kushuhudia walipoona mambo yaliyofanyika, walirudi huku wakipiga vifua vyao.
49 Lakini marafiki zake, na wanawake waliomfuata toka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiangalia hayo mambo.
50 Tazama, palikuwepo na mtu aitwaye Yusufu, ambaye ni mmoja wa baraza, mtu mzuri na mwenye haki,
51 (alikuwa hajakubaliana na maamuzi au matendo yao), kutoka Armathaya, mji wa Kiyahudi, ambao ulikua ukisubiria ufalme wa Mungu.
52 Mtu huyu, alimkaribia Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
53 Alimshusha, na akauzungushia sanda, na akaumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika jiwe, ambalo hakuna aliyewahi kuzikwa.
Luka 23 in Biblia ya Kiswahili