Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Luka 22:47-69 in Swahili (individual language)

Help us?

Luka 22:47-69 in Biblia Takatifu

47 Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu.
48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?”
49 Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, “Bwana, tutumie panga zetu?”
50 Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la kulia.
51 Hapo, Yesu akasema, “Acha! Hii inatosha.” Akaligusa sikio la mtu huyo akaliponya.
52 Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja kumkamata: “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi?
53 Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza.”
54 Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali.
55 Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao.
56 Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, “Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu.”
57 Lakini Petro akakana akisema, “Wee! simjui mimi.”
58 Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, “Wewe ni mmoja wao.” Lakini Petro akajibu “Bwana we; si mimi!”
59 Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, “Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati.”
60 Lakini Petro akasema, “Bwana wee; sijui hata unachosema!” Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika.
61 Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: “Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
62 Hapo akatoka nje, akalia sana.
63 Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki.
64 Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, “Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!”
65 Wakamtolea maneno mengi ya matusi.
66 Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo.
67 Nao wakamwambia, “Twambie! Je, wewe ndiwe Kristo?” Lakini Yesu akawaambia, “Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki;
68 na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu.
69 Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi.”
Luka 22 in Biblia Takatifu

Luka 22:47-69 in Biblia ya Kiswahili

47 Wakati alipokuwa bado akiongea, tazama, kundi kubwa la watu likatokea, na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili akiwaongoza. Akaja karibu na Yesu ili ambusu,
48 lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49 Wakati wale waliokuwa karibu na Yesu walipoona hayo yanayotokea, wakasema, “Bwana, je tuwapige kwa upanga?”
50 Kisha mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio lake la kulia.
51 Yesu akasema, “hii inatosha. Na akagusa sikio lake, akamponya.
52 Yesu akasema kwa kuhani mkuu, na kwa wakuu wa hekalu, na kwa wazee waliokuja kinyume chake, “Je mnakuja kana kwamba mnakuja kupambana na mnyang'anyi, na marungu na mapanga?
53 Nilipokuwa pamoja nanyi siku zote kwenye hekalu, hamkuweka mikono yenu juu yangu. Lakini hii ni saa yako, na mamlaka ya giza.”
54 Wakamkamata, wakamuongoza, wakamleta nyumbani mwa kuhani mkuu. Lakini Petro akamfuatilia kwa mbali.
55 Baada ya kuwa wamewasha moto katika ule uwanda wa ndani na walipokwisha kukaa chini pamoja, Petro akakaa katikati yao.
56 Mtumishi mmoja wa kike akamuona Petro alipokuwa amekaa katika mwanga utokanao na moto, akamtazama akamwambia, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja naye.”
57 Lakini Petro akakana, akasema, “mwanamke, mimi simjui.”
58 Baada ya muda kidogo, mtu mwingine akamuona akasema “Wewe pia ni mmoja wao”. Lakini Petro akajibu, “Mwanaume, mimi siyo.”
59 Baada ya kama saa moja hivi, mwanaume mmoja akasisitiza akasema, “Kweli kabisa huyu mtu pia alikuwa pamoja naye, maana ni Mgalilaya.”
60 Lakini Petro akasema, “Mwanaume, sijui usemalo.” Na mara, wakati akiongea, jogoo akawika.
61 Akageuka, Bwana akamtazama Petro. Na Petro akalikumbuka neno la Bwana, pale alipomwambia, “Kabla ya jogoo kuwika leo, utanikana mimi mara tatu.”
62 Akienda nje, Petro akalia kwa uchungu mwingi.
63 Kisha wale wanaume waliokuwa wakimlinda Yesu, wakamdhihaki na kumpiga.
64 Baada ya kumfunika macho, wakamuuliza, wakisema, “Tabiri! Ni nani aliyekupiga?”
65 Wakaongea mambo mengine mengi kinyume cha Yesu na kumkufuru yeye.
66 Mara ilipokuwa asubuhi, wazee wa watu walikusanyika pamoja, wakuu wa makuhani na waandishi. Wakampeleka kwenye Baraza,
67 wakisema, “Kama wewe ni Kristo, tuambie.” Lakini yeye akawaambia, “Kama nikiwaambia, hamtaniamini,
68 na kama nikiwauliza hamtanijibu.”
69 Lakini kuanzia sasa na kuendelea, Mwana wa Adamu atakuwa amekaa mkono wa kuume wa nguvu ya Mungu.”
Luka 22 in Biblia ya Kiswahili