Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Luka 22:3-32 in Swahili (individual language)

Help us?

Luka 22:3-32 in Biblia Takatifu

3 Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwae Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili.
4 Yuda akaenda akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa Hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao.
5 Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha.
6 Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua.
7 Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa.
8 Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.”
9 Nao wakamwuliza, “Unataka tuiandae wapi?”
10 Akawaambia, “Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia.
11 Mwambieni mwenye nyumba: Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?
12 Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo.”
13 Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka.
14 Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake.
15 Akawaambia, “Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu.
16 Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika Ufalme wa Mungu.”
17 Kisha akatwaa kikombe, akashukuru akasema, “Pokeeni, mgawanye ninyi kwa ninyi.
18 Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19 Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.”
20 Akafanya vivyo hivyo na kikombe, baada ya chakula, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu.
21 “Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani.
22 Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti.”
23 Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo.
24 Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu zaidi kuliko wengine.
25 Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu.
26 Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi.
27 Kwa maana, ni nani aliye mkuu: yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi.
28 “Ninyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu;
29 na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi Ufalme, vivyo hivyo nami nitawakabidhi ninyi Ufalme.
30 Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na mtaketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
31 “Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta ninyi kama mtu anavyopepeta ngano.
32 Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.”
Luka 22 in Biblia Takatifu

Luka 22:3-32 in Biblia ya Kiswahili

3 Shetani akaingia ndani ya Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na mbili.
4 Yuda akaenda kujadiliana na wakuu wa makuhani na wakuu namna ambavyo atamkabidhi Yesu kwao.
5 Walifurahi, na kukubaliana kumpa fedha.
6 Yeye aliridhia, na alitafuta fursa ya kumkabidhi Yesu kwao mbali na kundi la watu.
7 Siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika, ambapo kondoo wa Pasaka lazima atolewe.
8 Yesu akawatuma Petro na Yohana, akasema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuje tukile.”
9 Wakamuuliza, “Wapi unataka tuyafanyie hayo maandalizi?”
10 Akawajibu, “Sikilizeni, mtakapokuwa mmeingia mjini, mwanamume ambaye amebeba mtungi wa maji atakutana na ninyi. Mfuateni kwenye nyumba ambayo ataingia.
11 Kisha mwambieni bwana wa nyumba, “Mwalimu anakwambia, “Kiko wapi chumba cha wageni, mahali ambapo nitakula Pasaka na wanafunzi wangu?”
12 Atawaonyesha chumba cha ghorofani ambacho kiko tayari. Fanyeni maandalizi humo.”
13 Hivyo wakaenda, na wakakuta kila kitu kama alivyowaambia. Kisha wakaandaa chakula cha Pasaka.
14 Muda ulipofika alikaa na wale mitume.
15 Kisha akawaambia, “Nina shauku kubwa ya kula sikukuu hii ya Pasaka na ninyi kabla ya kuteswa kwangu.
16 Kwa maana nawaambieni, sitakula tena mpaka itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.”
17 Kisha Yesu akachukua kikombe, na alipokwisha kushukuru, akasema, “Chukueni hiki, na mgawane ninyi kwa ninyi.
18 Kwa maana nawaambia, sitakunywa tena mzao wa mzabibu, mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19 Kisha akachukua mkate, na alipokwisha kushukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu ambao umetolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.”
20 Akachukua kikombe vivyo hivyo baada ya chakula cha usiku akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, ambayo imemwagika kwa ajili yenu.
21 Lakini angalieni. Yule anisalitie yuko pamoja nami mezani.
22 Kwa maana Mwana wa Adamu kwa kweli aenda zake kama ilivyokwisha amuliwa. Lakini ole kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu asalitiwa!”
23 Wakaanza kuulizana wao kwa wao, nani miongoni mwao ambaye angefanya jambo hili.
24 Kisha yakatokea mabishano katikati yao kwamba ni nani anaye dhaniwa kuwa mkuu kuliko wote.
25 Akawaambia, “Wafalme wa watu wa mataifa wana ubwana juu yao, na wale mwenye mamlaka juu yao wanaitwa waheshimiwa watawala.
26 Lakini haitakiwi kabisa kuwa hivi kwenu ninyi. Badala yake, acha yule ambaye ni mkubwa kati yenu awe kama mdogo. Na yule ambaye ni wa muhimu sana awe kama atumikaye.
27 Kwa sababu yupi mkubwa, yule akaaye mezani au yule anayetumika? Je si yule aketie mezani? Na mimi bado ni kati yenu kama atumikaye.
28 Lakini ninyi ndio ambao mmeendelea kuwa nami katika majaribu yangu.
29 Nawapa ninyi ufalme, kama vile Baba alivyonipa mimi ufalme,
30 kwamba mpate kula na kunywa mezani kwangu kwenye ufalme wangu. Na mtakaa kwenye viti vya enzi mkizihukumu kabila kumi na mbili za Israel.
31 Simoni, Simoni, fahamu kwamba, Shetani ameomba awapate ili awapepete kama ngano.
32 Lakini nimekuombea, kwamba imani yako isishindwe. Baada ya kuwa umerudi tena, waimarishe ndugu zako.”
Luka 22 in Biblia ya Kiswahili