Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Filemoni

Filemoni 1

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na ndugu Timotheo kwa Filemoni, mpendwa rafiki yetu na mtenda kazi pamoja nasi,
2na kwa Afia dada yetu, na kwa Arkipas askari mwenzetu, na kwa kanisa lile linalokutana nyumbani kwako.
3Neema iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
4Wakati wote namshukuru Mungu. Ninakutaja katika maombi yangu.
5Nimesikia upendo na imani uliyonayo katika Bwana Yesu na kwa ajili ya waumini wote.
6Ninaomba kwamba ushirika wa imani yenu iwe na ufanisi katika ujuzi wa kila jambo jema lililoko kati yetu katika Kristo.
7Kwa kuwa nimekuwa na furaha na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa sababu mioyo ya waumini imekuwa ikitulizwa nawe, ndugu.
8Kwa hiyo, ingawa nina ujasiri wote katika Kristo kukuamuru wewe kufanya kile unachoweza kufanya,
9lakini kwa sababu ya upendo, badala yake nakusihi - mimi, Paulo niliye mzee, na sasa ni mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu.
10Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesmo, niliyemzaa katika vifungo vyangu.
11Kwa kuwa mwanzoni hakukufaa, lakini sasa anakufaa wewe na mimi.
12Nimemtuma- yeye ambaye ni wa moyo wangu hasa - kurudi kwako.
13Nataraji angeendelea kubaki pamoja nami, ili anitumikie badala yako, wakati niwako kifungoni kwa ajili ya injili.
14Lakini sikutaka kufanya jambo lolote bila ruhusa yako. Nilifanya hivi ili kwamba jambo lolote zuri lisifanyike kwa sababu nilikulazimisha, bali kwa sababu ulipenda mwenyewe kulitenda.
15Labda ni sababu alitengwa nawe kwa muda, ilikuwa hivyo ili uwe pamoja naye milele.
16Ili kwamba asiwe tena mtumwa, bali bora zaidi ya mtumwa, kama ndugu mpendwa, hasa kwangu, na zaidi sana kwako, katika mwili na katika Bwana.
17Na hivyo kama wanichukulia mimi mshirika, mpokee kama ambavyo ungenipokea mimi.
18Lakini kama amekukosea jambo lolote, au unamdai kitu chochote, kidai hicho kutoka kwangu.

19Mimi Paulo, ninaandika kwa mkono wangu mwenyewe: mimi nitakulipa. Sisemi kwako kwamba nakudai maisha yako hasa.
20Naam ndugu, acha nipate furaha ya Bwana toka kwako: uburudishe moyo wangu katika Kristo.
21Nikiwa na imani kuhusu utii wako, nakuandikia nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya vile ninavyokuomba.
22Wakati huo huo andaa chumba cha wageni kwa ajili yangu, kwa kuwa ninatumaini kupitia maombi yako nitakutembelea hivi karibuni.
23Epafra, mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu anakusalimu,
24na kama afanyavyo Marko, Aristarko, Dema, Luka, watendakazi pamoja nami.
25Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho yako. Amina.