1Nataka ninyi mjue kaka na dada zangu, ya kuwa baba zetu walikuwa chini ya wingu na wote walipita katika bahari.
2Wote walibatizwa wawe wa Musa ndani ya wingu na ndani ya bahari,
3na wote walikula chakula kile kile cha roho.
4Wote walikunywa kinywaji kile kile cha roho. Maana walikunywa kutoka katika mwamba wa roho uliowafuata, na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.
5Lakini Mungu hakupendezwa sana na wengi wao, na maiti zao zilisambazwa jangwani.
6Basi mambo haya yote yalikuwa mifano kwetu, ili sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya kama na wao walivyofanya.
7Msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa. Hii ni kama ilivyoandikwa, “Watu walikaa chini wakila na kunywa, na waliinuka kucheza kwa tamaa za mapenzi.”
8Tusifanye uasherati kama wengi wao walivyofanya. Wakafa siku moja watu ishirini na tatu elfu kwa sababu hiyo.
9Wala tusimjaribu Kristo, kama wengi wao walivyofanya na wakaharibiwa kwa nyoka.
10Na pia msinung'unike, kama wengi wao walivyonung'unika na kuharibiwa na malaika wa mauti.
11Basi mambo hayo yalitendeka kama mifano kwetu. Yakaandikwa ili kutuonya sisi - tuliofikiliwa na miisho ya zamani.
12Kwa hiyo kila ajionaye amesimama awe makini asije akaanguka.
13Hakuna jaribu lililowapata ninyi lisilo kawaida ya wanadamu. Ila Mungu ni mwaminifu. Hatawaacha mjaribiwe kupita uwezo wenu. Pamoja na jaribu yeye atawapa mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.
14Kwa hiyo, wapendwa wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.
15Nasema nanyi kama watu wenye akili, ili muamue juu ya ninalosema.
16Kikombe cha baraka tubarikicho, si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?
17Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja. Sisi sote twapokea mkate mmoja kwa pamoja.
18Watazameni watu wa Israeli: Je! Wale wote walao dhabihu si washiriki katika madhabahu?
19Nasema nini basi? Ya kuwa sanamu ni kitu? Au ya kuwa chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu?
20Lakini nasema juu ya vitu vile wavitoavyo sadaka watu wapagani wa Mataifa, ya kuwa wanatoa vitu hivi kwa mapepo na sio kwa Mungu. Nami sitaki ninyi kushirikiana na mapepo!
21Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mapepo. Hamwezi kuwa na ushirika katika meza ya Bwana na katika meza ya mapepo.
22Au twamtia Bwana wivu? Tuna nguvu zaidi yake?
23“Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vifaavyo. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote viwajengavyo watu.
24Hakuna hata mmoja angetafuta mazuri yake tu. Badala yake, kila mmoja angetafuta mazuri ya mwenzake.
25Mnaweza kula kila kitu kiuzwacho sokoni bila kuuliza -uliza kwa ajili ya dhamiri.
26Maana “dunia ni mali ya Bwana, na vyote viijazavyo.”
27Na mtu asiyeamini akiwaalika kula, na mnataka kwenda, kuleni chochote awapacho pasipo kuuliza maswali ya dhamiri.
28Lakini mtu akiwaambia, “Chakula hiki kimetokana na sadaka ya wapagani,” msile. Hii ni kwa ajili yake aliyewaambia, na kwa ajili ya dhamiri.
29Nami simaanishi dhamiri zenu, bali dhamiri ya yule mwingine. Maana kwanini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?
30Ikiwa mimi natumia chakula kwa shukrani, kwanini nitukanwe kwa kitu ambacho nimeshukuru kwacho?
31Kwa hiyo, chochote mnachokula au kunywa, au chochote mfanyacho, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
32Msiwakoseshe Wayahudi au Wayunani, au kanisa la Mungu.
33Jaribuni kama mimi ninavyojaribu kuwapendeza watu wote kwa mambo yote. Sitafuti faida yangu mwenyewe, bali ya wengi. Nami nafanya hivi ili wapate kuokolewa.