1 Ee Yahwe, wewe umenichunguza, na unanijua.
2 Wewe unajua nikaapo na niinukapo; unayajua mawazo yangu tokea mbali sana.
3 Unachunguza wenendo wangu na kulala kwangu; unazijua njia zangu zote.
4 Kabla hakujawa na neno kwenye ulimi wangu, wewe unalijua kabisa, Yahwe.
5 Nyuma yangu na mbele yangu unanizunguka na kuniwekea mkono wako.
6 Maarifa hayo ni mengi yananizidi mimi; yako juu sana, nami siwezi kuyafikia.
7 Niende wapi mbali na roho yako? Niende wapi niukimbie uwepo wako?
8 Kama nikipaa mbinguni, uko huko; kama nikifanya kitanda changu Kuzimuni, tazama, uko huko.
9 Kama nikipaa kwa mbawa za asubuhi na kwenda kuishi pande za mwisho wa bahari,
10 hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika.
11 Kama nikisema, “Hakika giza litanifunika, na nuru inizungukayo itakuwa usiku,”
12 Hata giza lisingweza kuwa giza kwako. Usiku ungeng'aa kama mchana, maana giza na nuru kwako vinafanana.