Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Zaburi 119:108-173 in Swahili (individual language)

Help us?

Zaburi 119:108-173 in Biblia ya Kiswahili

108 Yahwe, tafadhali pokea dhabihu yangu ya hiari ya kinywa changu, na unifundishe amri zako za haki.
109 Uhai wangu ziku zote uko mkononi mwangu, lakini bado sisahau sheria yako.
110 Waovu wamenitegea mtego, lakini sijapotea mbali na maagizo yako.
111 Nimezifanya amri za agano lako kama urithi wangu milele, maana hizo ni furaha ya moyo wangu.
112 Moyo wangu umewekwa kuzitii sheria zako milele mpaka mwisho kabisa. SAMEKH.
113 Ninawachukia watu wa kusita-sita, lakini naipenda sheria yako.
114 Wewe ni ficho langu na ngao yangu; nalingoja neno lako.
115 Ondokeni kwangu, ninyi mtendao uovu, ili niweze kuzitii amri za Mungu wangu.
116 Uniwezeshe kwa neno lako ili niweze kuishi na nisiaibike na matumaini yangu.
117 Unisaidie, nami nitakuwa salama; siki zote nitazitafakari sheria zako.
118 Wewe huwakataa wale wote wapoteao mbali na sheria zako, maana watu hao ni wadanganyifu na si wakuaminika.
119 Wewe huwaondoa waovu wa nchi kama takataka; kwa hiyo ninazipenda amri zako thabiti.
120 Mwili wangu hutetemeka kwa hofu yako, na ninaziogopa amri za haki yako. AYIN.
121 Ninafanya kilicho sahihi na haki; usiniache kwa watesi wangu.
122 Uwe mdhamini wa ustawi wa mtumishi wako; usiwaache wenye kiburi wanionee.
123 Macho yangu yanachoka kwa kuusubiri wokovu wako na neno lako la haki.
124 Mwoneshe mtumishi wako uaminifu wa agano lako, na unifundishe sheria zako.
125 Mimi ni mtumishi wako; unipe uelewa ili niweze kuzijua amri za agano lako.
126 Ni wakati wa Yahwe kutenda, kwa maana watu wamevunja sheria yako.
127 Hakika ninazipenda amri zako kuliko dhahabu, naam, kuliko dhahabu safi.
128 Hivyo ninayafuata maagizo yako yote kwa makini, na ninachukia kila njia ya uongo. PE.
129 Sheria zako ni za ajabu, ndiyo sababu ninazitii.
130 Ufafanuzi wa maneno yako huleta nuru; na kumpa ufahamu mjinga.
131 Ninafungua kinywa changu na kutweta, maana ninazitamani amri zako.
132 Unigeukie na unihurumie, kama ufanyavyo siku zote kwa wale walipendao jina lako.
133 Uziongoze hatua zangu kwa neno lako; usiruhusu dhambi yeyote initawale.
134 Unikomboe dhidi ya wanadamu waonevu ili niyatii maagizo yako.
135 Uso wako umwangazie mtumishi wako, na unifundishe sheria zako.
136 Mito ya machozi yatiririka kutoka machoni pangu kwa sababu watu hawaitii sheria yako. TSADHE.
137 Wewe ni mwenye haki, Yahwe, na amri zako ni haki.
138 Umezipa amri za agano lako haki na uaminifu.
139 Hasira imeniangamiza kwa sababu adui zangu husahau maneno yako.
140 Neno lako limepimwa sana, naye mtumishi wako analipenda.
141 Sina umuhimu na ninadharauliwa, lakini bado siyasahau maagizo yako.
142 Hukumu yako ni ya haki milele, na sheria yako ni ya kuaminika.
143 Japo dhiki na taabu vimenipata, amri zako bado ni furaha yangu.
144 Amri za agano lako ni za haki milele; unipe uelewa ili niweze kuishi. QOPH.
145 Nililia kwa moyo wangu wote, “Unijibu, Yahwe, nitazishika sheria zako.
146 Ninakuita wewe; uniokoe, nami nitazitii amri za agano lako.”
147 NInaamka asubuhi kabla jua halijachomoza na kulia kwa ajili ya msaada.
148 Ninatumaini katika maneno yako. Macho yangu yako wazi usiku kucha ili niweze kutafakari juu ya neno lako.
149 Sikia sauti yangu katika uaminifu wa agano lako; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika amri zako za haki.
150 Wale wanaonitesa wananikaribia, lakini wako mbali na sheria yako.
151 Wewe uko karibu, Yahwe, na amri zako ni za kuaminika.
152 Muda mrefu uliopita nilijifunza kutoka katika amri za agano lako ulizoziweka katika mahali pa milele. RESH.
153 Uyatazame mateso yangu na unisaidie, maana siisahau sheria yako.
154 Unitetee na kunikomboa; unihifadhi, kama ulivyo ahidi katika neno lako.
155 Wokovu uko mbali na waovu, maana hawazipendi amri zako.
156 Matendo yako ya huruma ni makuu, Yahwe; uniweke hai; kama ufanyavyo siku zote.
157 Watesi wangu na adui zangu ni wengi, lakini bado sijaenda mbali na amri za agano lako.
158 Nimewaona wasaliti wakitia kinyaa kwa sababu hawalishiki neno lako.
159 Tazama jinsi niyapendavyo maagizo yako; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika uaminifu wa agano lako.
160 Kiini cha neno lako ni kweli; kila mmoja mwenye amri za haki hudumu milele. SHIN.
161 Wakuu hunitesa bila sababu; moyo wangu hutetemeka, ukiogopa kutolitii neno lako.
162 Ninalifurahia neno lako kama apataye nyara nyingi.
163 Ninachukia na kudharau uongo, lakini naipenda sheria yako.
164 Mara saba kwa siku ninakusifu wewe kwa sababu ya amri zako za haki.
165 Wana amani nyingi, waipendao sheria yako; hakuna cha kuwatia mashakani.
166 Naungoja wokovu wako, Yahwe, na ninatii amri zako.
167 Ninazishika amri zako thabiti, na ninazipenda sana.
168 Ninayashika maagizo yako na amri zako thabiti, kwa maana unajua kila kitu nifanyacho. TAV.
169 Sikia kilio changu, Yahwe; unipe uelewa wa neno lako.
170 Maombi yangu yaje mbele zako; unisaidie, kama ulivyoahidi katika neno lako.
171 Midomo yangu na imwage sifa, maana wewe unanifundisha sheria zako.
172 Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, maana amri zako zote ni za haki.
173 Mkono wako unisaidie, maana nimechagua maagizo yako.
Zaburi 119 in Biblia ya Kiswahili