Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Zaburi - Zaburi 78

Zaburi 78:27-55

Help us?
Click on verse(s) to share them!
27Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, na ndege kama wingi wa mchanga wa baharini.
28Walianguka katikati ya kambi yao, na maeneo yote karibu na hema zao.
29Hivyo walikula na walishiba. Maana aliwapa kile walichokitamani sana.
30Lakini walikuwa bado hawajatosheka; chakula chao kilikuwa bado kinywani mwao.
31Ndipo hasira ya Mungu iliwashambulia na kuwaua wenye nguvu kati yao. Aliwaangusha chini vijana wa Israeli.
32Licha ya hili, waliendelea kutenda dhambi na hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.
33Hivyo Mungu alizikatisha siku zao; miaka yao ilijawa na hofu.
34Wakati wowote Mungu alipowataabisha, nao waligeuka na kumtafuta yeye kwa bidii.
35Walikumbuka kuwa Mungu alikuwa mwamba wao na kuwa Mungu Aliye Juu Sana alikuwa mwokozi wao.
36Lakini walimsifia tu kwa vinywa vyao na kumdanganya kwa maneno yao.
37Maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, na hawakuwa waaminifu kwa agano lake.
38Lakini yeye, kwa kuwa alikuwa alikuwa na huruma, aliwasamehe uovu wao na hakuwaangamiza. Ndiyo, wakati mwingi aliizuia hasira yake na hakuionesha ghadhabu yake yote.
39Alikumbuka kuwa waliumbwa kwa mwili, upepo ambao hupita nao haurudi.
40Mara ngapi wameasi dhidi yake jangwani na kumuhuzunisha nyikani!
41Tena na tena walimjaribu Mungu na wakamtilia mashaka Mtakatifu wa Israeli.
42Hawakufikiria kuhusu uweza wake, jinsi alivyo waokoa dhidi ya adui
43alipofanya ishara za kutisha katika Misri na maajabu yake katika konde la Soani.
44Aligeuza mito ya Wamisri kuwa damu ili wasipate kunywa kutoka katika vijito vyao.
45Alituma makundi ya inzi yaliyowavamia na vyura ambao walisambaa katika nchi yao.
46Aliwapa mazao yao panzi na kazi yao nzige.
47Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na miti ya mikuyu kwa mvua ya mawe zaidi.
48Aliinyeshea mifugo yao mvua ya mawe na alirusha radi ya umeme ikapiga mifugo yao. Ukali wa hasira yake ulielekea dhidi yao.
49Alituma gadhabu, uchungu na taabu kama wakala aletaye maafa.
50Aliifanyia njia hasira yake; hakuwakinga dhidi ya kifo bali aliwakabidhi kwa pigo.
51Aliwaua wazaliwa wote wa kwanza katika Misri, wazaliwa wa kwanza wa nguvu zao katika mahema ya Hamu.
52Aliwaongoza nje watu wake mwenyewe kama kondoo na aliwaelekeza kupitia jangwani kama kundi.
53Aliwaongoza salama na pasipo na woga, lakini bahari iliwaelemea adui zao.
54Kisha aliwaleta mpaka wa nchi yake takatifu, kwenye mlima huu ambao aliutwaa kwa mkono wake wa kuume.
55Aliwafukuza mataifa mbele yao na akawapa urithi wao. Aliwakalisha makabila ya Israeli katika mahema yao.

Read Zaburi 78Zaburi 78
Compare Zaburi 78:27-55Zaburi 78:27-55