Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Yohana - Yohana 8

Yohana 8:31-46

Help us?
Click on verse(s) to share them!
31Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
32Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.”
33Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: mtakuwa huru?”
34Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.
36Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.
37Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu.
38Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”
39Wao wakamjibu, “Baba yetu ni Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
40Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
41Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.”
42Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
44Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
45Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
46Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?

Read Yohana 8Yohana 8
Compare Yohana 8:31-46Yohana 8:31-46