Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Yohana - Yohana 7

Yohana 7:2-32

Help us?
Click on verse(s) to share them!
2Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
3Basi ndugu zake wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya.
4Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadam unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu.”
5(Hata ndugu zake hawakumwamini!)
6Basi, Yesu akawaambia, “Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa.
7Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu.
8Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika.”
9Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.
10Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.
11Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza: “Yuko wapi?”
12Kulikuwa na minong'ono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.”
13Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
14Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza kufundisha.
15Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?”
16Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
17Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
18Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.
19Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
20Hapo watu wakamjibu, “Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?”
21Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.
22Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato.
23Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato?
24Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.”
25Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu?
26Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?
27Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!”
28Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.
29Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.”
30Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
31Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?”
32Mafarisayo waliwasikia watu wakinong'ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.

Read Yohana 7Yohana 7
Compare Yohana 7:2-32Yohana 7:2-32