Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Yohana - Yohana 6

Yohana 6:9-50

Help us?
Click on verse(s) to share them!
9“Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?”
10Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume elfu tano.
11Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
12Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.”
13Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.
14Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.”
15Yesu akajua ya kuwa watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake.
16Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,
17wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado.
18Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
19Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.
20Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!”
21Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walipokuwa wanakwenda.
22Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao.
23Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.
24Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
25Wale watu walipomkuta Yesu ng'ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?”
26Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uzima wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.”
28Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?”
29Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini yule aliyemtuma.”
30Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?
31Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.”
32Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni.
33Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uzima.”
34Basi, wakamwambia, “Mheshimiwa, tupe daima mkate huo.”
35Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
36Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.
37Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,
38kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.
39Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho.
40Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho.”
41Basi, Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
42Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?”
43Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika ninyi kwa ninyi.
44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho.
45Manabii wameandika: Watu wote watafundishwa na Mungu. Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.
46Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
47Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele.
48Mimi ni mkate wa uzima.
49Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
50Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa.

Read Yohana 6Yohana 6
Compare Yohana 6:9-50Yohana 6:9-50