Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Yohana - Yohana 4

Yohana 4:3-24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
3Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;
4na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.
5Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.
6Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
7Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.”
8(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
9Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)
10Yesu akamjibu, “Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: Nipatie maji ninywe, ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai.”
11Huyo mama akasema, “Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?
12Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki.”
13Yesu akamjibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena.
14Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele.”
15Huyo mwanamke akamwambia, “Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji.”
16Yesu akamwambia, “Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa.”
17Huyo mwanamke akamwambia, “Mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli, kwamba huna mume.
18Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli.”
19Huyo Mwanamke akamwambia, “Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii.
20Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu.”
21Yesu akamwambia, “Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.
23Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka.
24Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake.”

Read Yohana 4Yohana 4
Compare Yohana 4:3-24Yohana 4:3-24