Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Warumi - Warumi 11

Warumi 11:3-36

Help us?
Click on verse(s) to share them!
3“Bwana, wamewaua manabii wako, nao wamebomoa madhabahu zako. Mimi peke yangu nimesalia, nao wanatafuta uhai wangu.”
4Lakini jibu la Mungu lasema nini kwako? “Nimetunza kwa ajili yangu watu elfu saba ambao hawampigii magoti Baali.”
5Hata hivyo, wakati huu wa sasa pia kuna walio salia kwa sababu ya uchaguzi wa neema.
6Lakini ikiwa ni kwa neema, si tena kwa matendo. Vinginevyo neema haitakuwa tena neema.
7Ni nini basi? Jambo ambalo Israeli alikuwa akitafuta, hakukipata, bali wateule walikipata, na wengine walitiwa uzito.
8Ni kama ilivyoandikwa: “Mungu amewapa roho ya ubutu, macho ili wasione, na masikio ili wasisikie, mpaka leo hii.”
9Naye Daudi anasema, “Acha meza zao na ziwe wavu, mtego, sehemu ya kujikwaa, na kulipiza kisasi dhidi yao.
10Acha macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona. Ukawainamishe migongo yao daima.”
11Basi nasema, “Je, wamejikwaa hata kuanguka?” Isiwe hivyo kamwe. Badala yake, kwa kushindwa kwao, wokovu umefika kwa Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.
12Sasa ikiwa kushindwa kwao ni utajiri wa ulimwengu, na kama hasara yao ni utajiri wa mataifa, ni kiasi gani zaidi itakuwa kukamilika kwao?
13Na sasa naongea nanyi watu wa Mataifa. Kwa kuwa nimekuwa mtume kwa watu wa Mataifa mengine, najivunia huduma yangu.
14Labda nitawatia wivu walio mwili mmoja na mimi. Labda tutawaokoa baadhi yao.
15Maana ikiwa kukataliwa kwao ni maridhiano ya dunia, kupokelewa kwao kutakuwaje ila uhai toka kwa wafu?
16Kama matunda ya kwanza ni akiba, ndivyo ilivyo kwa donge la unga. Kama mzizi ni akiba, matawi nayo kadhalika.
17Lakini kama baadhi ya matawi yamekatwa, kama wewe, tawi pori la mzeituni, ulipandikizwa kati yao, na kama ulishiriki pamoja nao katika mizizi ya utajiri wa mzeituni,
18usijisifu juu ya matawi. Lakini kama unajisifu, si wewe ambaye unaisaidia mizizi, bali mizizi inakusaidia wewe.
19Basi utasema, “Matawi yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika shina.”
20Hiyo ni kweli. Kwa sababu ya kutoamini kwao walikatwa, lakini wewe ulisimama imara kwa sababu ya imani yako. Usijifikirie mwenyewe kwa hali ya juu sana, bali ogopa.
21Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, hatakuhurumia wewe pia.
22Angalia, basi, matendo mema na ukali wa Mungu. Kwa upande mmoja, ukali ulikuja juu ya Wayahudi ambao walianguka. Lakini kwa upande mwingine, wema wa Mungu huja juu yako, kama utadumu katika wema wake. Vinginevyo wewe pia utakatiliwa mbali.
23Na pia, kama hawataendelea katika kutoamini kwao, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.
24Kwa maana ikiwa ninyi mlikatwa nje kwa ulio kwa asili mzeituni mwitu, na kinyume cha asili mlipandikizwa katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana hawa Wayahudi, ambao ni kama matawi ya asili kuweza kupandikizwa tena ndani ya mzeituni wao wenyewe?
25Kwa maana ndugu sitaki msijue, kuhusiana na siri hii, ili kwamba msiwe na hekima katika kufikiri kwenu wenyewe. Siri hii ni kwamba ugumu umetokea katika Israeli, hadi kukamilika kwa mataifa kutakapokuja.
26Hivyo Israeli wote wataokoka, kama ilivyoandikwa: “Kutoka Sayuni atakuja Mkombozi. Atauondoa uovu kutoka kwa Yakobo.
27Na hili litakuwa agano langu pamoja nao, wakati nitakapoziondoa dhambi zao.”
28Kwa upande mmoja kuhusu injili, wanachukiwa kwa sababu yenu. Kwa upande mwingine kutokana na uchaguzi wa Mungu, wamependwa kwa sababu ya mababu.
29Kwa kuwa zawadi na wito wa Mungu haubadiliki.
30Kwa kuwa awali ninyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmeipokea rehema kwa sababu ya kuasi kwao.
31Kwa njia iyo hiyo, sasa hawa Wayahudi wameasi. Matokeo yake ni kwamba kutokana na huruma mliyojaliwa ninyi wanaweza pia kupokea rehema.
32Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi, ili aweze kuwahurumia wote.
33Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hazichunguziki hukumu zake, na njia zake hazigunduliki!
34“Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani amekuwa mshauri wake?
35Au ni nani kwanza aliyempa kitu Mungu, ili alipwe tena?”
36Kwa maana kutoka kwake, na kwa njia yake na kwake, vitu vyote vipo. Kwake uwe utukufu milele. Amina.

Read Warumi 11Warumi 11
Compare Warumi 11:3-36Warumi 11:3-36