Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Warumi - Warumi 11

Warumi 11:2-24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
2Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Eliya wakati alipomnung'unikia Mungu kuhusu Israeli:
3“Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua?”
4Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: “Nimejiwekea elfu saba ambao hawakumwabudu Baali.”
5Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake.
6Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena.
7Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa,
8kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito, na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao wala kusikia kwa masikio yao.”
9Naye Daudi anasema: “Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa, waanguke na kuadhibiwa.
10Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona. Migongo yao ipindike kwa taabu daima!”
11Basi, nauliza: je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu.
12Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao kwa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri zaidi kwamba utimilifu wao utasababisha baraka nyingi zaidi.
13Basi, sasa nawaambieni ninyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu,
14nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee ninyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao.
15Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka!
16Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia.
17Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Ninyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini.
18Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si ninyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza ninyi.
19Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.”
20Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari.
21Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe?
22Kumbuka, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa.
23Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.
24Ninyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao.

Read Warumi 11Warumi 11
Compare Warumi 11:2-24Warumi 11:2-24