Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 1Samweli

1Samweli 11

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Ndipo Nahashi Mwamoni akaenda na kupiga kambi kuzunguka Yabeshi Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia,”
2Nahashi Mwamoni akawajibu, “Kwa sharti hili nitafanya mkataba na ninyi, kwamba wote niwang'oe macho ya kulia, na kwa kitendo hiki kilete fedheha katika Israeli yote.”
3Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, “Tuache kwa siku saba, ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Ndiposa, kama hakuna mtu wa kutuokoa, tutasalimu amri kwako.”
4Nao wajumbe wakafika Gibea, alipoishi Sauli, na wakawaeleza watu kile kilichotokea. Watu wote wakalia kwa sauti kuu.
5Na Sauli alikuwa akiwafuata nyuma maksai kutoka shambani. Sauli akauliza, “Watu wamepatwa na nini hadi wanalia?” Ndipo wakamweleza Sauli kile ambacho watu wa Yabeshi walikisema.
6Sauli aliposikia kile walichosema, Roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, na akakasirika.
7Akashika nira ya maksai, akawakata hao ng'ombe vipande vipande, na akavituma hivyo vipande katika nchi yote ya Israeli kwa kuwatumia wajumbe, Akasema, “Yeyote asiyejitokeza akimfuata Sauli na Samweli, hivi ndivyo ng'ombe wake watakavyofanywa.” Na hofu ya BWANA ikawaingia watu, na wakajitokeza wote kwa pamoja.
8Alipowahesabu hapo Beseki, watu wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na watu wa Yuda elfu thelathini.
9Wakawaambia wale wajumbe waliotumwa, “Mtawaambia watu wa Yabeshi Gileadi, 'Kesho, wakati wa jua kali, Mtaokolewa.”' Basi wale wajumbe wakaenda na kuwaambia watu wa Yabeshi, na watu wakafurahi.
10Ndipo watu wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, “Kesho tutasalimu amri kwako, na utaweza kutufanyia chochote unachoona kinakupendeza.”
11Siku iliyofuata Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu. Wakafika katikati ya Kambi wakati wa asubuhi, wakawashambulia na kuwashinda Waamoni ilipofika mchana. Waliosalimika nao walitawanyika, kiasi kwamba hata watu wawili hawakuachwa pamoja.
12Ndipo watu wakamwambia Samweli, “Wako wapi waliosema, 'Hivi kweli Sauli atatutawala?' Walete watu hao, ili tuwauwe.”
13Lakini Sauli akasema, “Hakuna atakayeuwawa siku ya leo, kwa sababu leo BWANA amemuokoa Isreli.”
14Kisha Samweli akawaambia watu, “Njoni, twendeni Gilgali na tuimarishe ufalme tena huko.”
15Hivyo watu wote wakaenda Gilgali na wakamsimika Sauli kuwa mfalme mbele za BWANA huko Gilgali. Na huko walitoa sadaka za amani mbele za BWANA, na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.