Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Wagalatia

Wagalatia 2

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Baada ya miaka kumi na nne nilienda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba. Pia nilimchukua Tito pamoja nami.
2Nilienda kwa sababu Mungu alijidhihirisha kwangu kwamba nilipaswa kwenda. Niliweka mbele yao Injili ambayo niliitangaza kwa watu wa mataifa. (Lakini niliongea kwa siri kwa waliosemekana kuwa viongozi muhimu). Nilifanya hivi ili kuhakikisha kwamba nilikuwa sikimbii, au nilikimbia bure.
3Lakini hata Tito, aliyekuwa pamoja nami, aliyekuwa Myunani, alilazimishwa kutahiriwa.
4Jambo hili lilitokea kwa sababu ya ndugu wa uongo waliokuja kwa siri kupeleleza uhuru tuliokuwa nao katika Kristo Yesu. Walitamani kutufanya sisi kuwa watumwa wa sheria.
5Hatukujitoa kuwatii hata kwa saa moja, ili kwamba injili ya kweli ibaki bila kubadilika kwenu.
6Lakini wale waliosemwa kuwa walikuwa viongozi hawakuchangia chochote kwangu. Chochote walichokuwa wakikifanya hakikuwa na maana kwangu. Mungu hakubali upendeleo wa wanadamu.
7Badala yake, waliniona kwamba nimeaminiwa kuitangaza injili kwa wale ambao hawakutahiriwa. Ilikuwa kama Petro atangaze injili kwa waliotahiriwa.
8Kwa maana Mungu, aliyefanya kazi ndani ya Petro kwa ajili ya utume kwa wale waliotahiriwa, pia alifanya kazi ndani yangu kwa watu wa mataifa.
9Wakati Yakobo, Kefa, na Yohana, waliotambulika kuwa waliojenga Kanisa, walifahamu neema niliyopewa mimi, walitupokea katika ushirika mimi na Barnaba. Walifanya hivi ili kwamba twende kwa watu wa mataifa, na ili kwamba waweze kwenda kwa wale waliotahiriwa.
10Pia walitutaka sisi kuwakumbuka masikini. Mimi pia nilikuwa natamani kufanya jambo hili.
11Wakati Kefa alipokuja Antiokia, nilimpinga waziwazi kwa sababu alikuwa amekosea.
12Kabla ya watu kadhaa kuja kutoka kwa Yakobo, Kefa alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa. Lakini hawa watu walipokuja, aliacha na kuondoka kutoka kwa watu wa mataifa. Alikuwa anaogopa watu ambao walihitaji tohara.
13Vilevile Wayahudi wengine waliungana na unafiki huu pamoja na Kefa. Matokeo yake yalikuwa kwamba hata Barnaba alichukuliwa na unafiki wao.
14Lakini nilipoona kwamba walikuwa hawafuati injili ya kweli, nilimwambia Kefa mbele yao wote, “Kama ninyi ni Wayahudi lakini mnaishi tabia za watu wa mataifa badala ya tabia za Kiyahudi, kwa nini mnawalazimisha watu wa mataifa kuishi kama Wayahudi?”
15Sisi ambao ni Wayahudi kwa kuzaliwa na siyo “Watu wa mataifa wenye dhambi”
16fahamu kwamba hakuna anayehesabiwa haki kwa matendo ya sheria. Badala yake, wanahesabiwa haki kwa imani ndani ya Yesu Kristo. Tulikuja kwa imani ndani ya Kristo Yesu ili kwamba tunahesabiwa haki kwa imani ndani ya Kristo na siyo kwa matendo ya sheria. Kwa matendo ya sheria hakuna mwili utakao hesabiwa haki.
17Lakini kama tunapomtafuta Mungu kwa kutuhesabia haki ndani ya Kristo, tunajikuta wenyewe pia kuwa wenye dhambi, je Kristo alifanywa mtumwa wa dhambi? Siyo hivyo!
18Maana kama nikijenga tegemeo langu juu ya kutunza sheria, tegemeo ambalo nilikwisha liondoa, najionesha mwenyewe kuwa mvunja sheria.

19Kupitia sheria nilikufa kwa sheria, kwa hiyo napaswa kuishi kwa ajili ya Mungu.
20Nimesulubiwa pamoja na Kristo. Si mimi tena ninayeishi, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha ninayoishi katika mwili ninaishi kwa imani ndani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda na akajitoa kwa ajili yangu.
21Siikani neema ya Mungu, maana kama haki ilikuwepo kupitia sheria, basi Kristo angekuwa amekufa bure.