Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Matendo ya Mitume

Matendo ya Mitume 26

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Hivyo, Agripa akamwambia Paulo, `Unaruhusiwa kujitetea.' Ndipo Paulo akanyoosha mkono wake akajitetea hivi.
2“Najiona mwenye furaha, Mfalme Agripa, ili kufanya kesi yangu mbele yako leo dhidi ya mashtaka yote ya Wayahudi.
3Hasa, kwa sababu wewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na maswali. Hivyo naomba unisikilize kwa uvumilivu.
4Kweli, Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu ujana wangu katika taifa langu huko Yerusalemu.
5Wananijua tangu mwanzo na wanapaswa kukubali kwamba niliishi kama Mfarisayo, dhehebu lenye msimamo mkali kwenye dini yetu.
6Sasa nimesimama hapa nihukumiwe kwa sababu mimi naliangalia ahadi ambayo Mungu aliifanya na baba zetu.
7Hii ni ahadi ambayo makabila yetu kumi na mbili yanatumaini kupokea kama wakimwabudu Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ni kwa ajili ya tumaini hili, mfalme Agripa, kwamba Wayahudi wananishitaki.
8Kwa nini yeyote kati yenu anafikiri ni ajabu kwamba Mungu hufufua wafu?
9Wakati mmoja nilifikiria mwenyewe kwamba ningefanya mambo mengi dhidi ya jina la Yesu wa Nazareti.
10Nilifanya haya katika Yerusalemu; Niliwafunga waamini wengi gerezani, na nilikuwa na mamlaka kutoka kwa wakuu wa makuhani kufanya hivyo; na wakati wanauawa, nilipiga kura dhidi yao.
11Mara nyingi niliwaadhibu katika masinagogi yote na nilijaribu kuwafanya waikane imani yao. Nilikuwa na hasira sana juu yao na niliwafukuza hata katika miji ya ugenini.
12Wakati nilipokuwa nikifanya haya, nilienda Dameski, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu;
13nilipokuwa njiani wakati wa mchana, Mfalme, niliona mwanga kutoka mbinguni uliokuwa mkali kuliko jua na uling'aa kutuzunguka mimi na watu waliokuwa wakisafiri pamoja nami.
14Sisi sote tulipoanguka chini, nalisikia sauti ikizungumza na mimi ikisema katika lugha ya Kiebrania: `Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.
15Ndipo nikasema, 'Wewe ni nani, Bwana?' Bwana akajibu, 'Mimi ni Yesu ambaye unanitesa.
16Sasa inuka usimame kwa miguu yako; sababu kwa kusudi hili mimi nimeonekana kwako, nimekuteua kuwa mtumishi na shahidi juu ya mambo ambayo unajua kuhusu mimi sasa na mambo nitakayokuonyesha baadaye;
17na Nitakuokoa kutoka kwa watu na watu wa Mataifa ambapo ninakutuma,
18kufungua macho yao na kuwatoa gizani kwenda kwenye mwanga na kutoka kwenye nguvu za shetani wamgeukie Mungu; ili wapate kupokea kutoka kwa Mungu msamaha wa dhambi na urithi ambao nimewapa wale niliowatenga kwa imani iliyo kwangu.

19Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuasi maono ya mbinguni,
20lakini, kwa wale walio katika Dameski kwanza, na kisha Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine, nilihubiri kwamba watubu na kumgeukia Mungu, wafanye matendo yanayostahili toba.
21Kwa sababu hiyo Wayahudi walinikamata hekaluni, wakajaribu kuniua.
22Mungu amenisaidia mpaka sasa, hivyo nasimama na kushuhudia kwa watu wa kawaida na kwa wale wakubwa juu ya yale ambayo manabii na Musa walisema yatatokea na si vingine;
23kwamba Kristo lazima atateseka na atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu na kutangaza mwanga kwa Wayahudi na watu wa mataifa.
24Paulo alipomaliza kujitetea, Festo alisema kwa sauti kubwa, 'Paulo, wewe ni mwendawazimu! masomo yako yamekufanya uwe mwendawazimu.
25Lakini Paulo akasema, Mimi si mwendawazimu, mheshimiwa Festo; lakini kwa ujasiri nasema maneno ya ukweli mtupu.
26Kwa kuwa mfalme anajua kuhusu mambo haya; na hivyo, ninaongea kwa uhuru kwake, kwa maana nina hakika kwamba hakuna lolote lililofichwa kwake; kwa kuwa hili halijafanywa pembeni.
27Je, unaamini manabii, Mfalme Agripa? Najua kwamba unaamini.'
28Agripa akamwambia Paulo, 'Kwa muda mfupi unaweza kunishawishi mimi na kunifanya Mkristo?
29Paulo akasema, '“Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu, bali pia wote wanaonisikia leo, wawe kama mimi, lakini bila hii minyororo ya gerezani.”
30Ndipo mfalme alisimama, na liwali, na Bernike pia, na wale waliokuwa wamekaa pamoja nao,
31walipoondoka ukumbini, walizungumzia wao kwa wao na kusema, 'Mtu huyu hastahili kifo wala kifungo.'
32Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kuwekwa huru kama asingekata rufani kwa Kaisari.”