Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Marko

Marko 15

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Asubuhi na mapema wakuu wa makuhani walikutana pamoja na wazee na waandishi na baraza zima la wazee. Kisha wakamfunga Yesu wakampeleka kwa Pilato. Pilato akamwuliza, “wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
2“Akamjibu, “Wewe umesema hivyo.”
3Wakuu wa makuhani wakaeleza mashitaka mengi juu ya Yesu.
4Pilato akamwuliza tena, “Hujibu chochote? Huoni jinsi wanavyokushtaki kwa mambo mengi?
5Lakini Yesu hakumjibu Pilato, na hiyo ilimshangaza.
6Kwa kawaida wakati wa sikukuu humfungulia mfungwa mmoja, mfungwa waliyemwomba.
7Kulikuwapo wahalifu gerezani, miongoni mwa wauaji kati ya walioasi wanaotumikia makosa yao. Alikuwepo mtu mmoja aitwaye Baraba.
8Umati ulikuja kwa Pilato, na kumwomba afanye kama alivyofanya huko nyuma.
9Pilato akawajibu na kusema, “Mnataka niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?”
10Kwa kuwa alijua ni kwa sababu ya wivu wakuu wa makuhani walimkamata Yesu na kumleta kwake.
11Lakini wakuu wa makuhani walichochea umati kupiga kelele kwa sauti kwamba afunguliwe Baraba badala yake.
12Pilato akawajibu tena na kusema, “Nimfanye nini Mfalme wa Wayahudi?
13Wakapiga kelele tena, “Msulibishe!”
14Pilato akasema, “Amefanya jambo gani baya?” Lakini wakazidi kupiga kelele zaidi na zaidi “Msulibishe.”
15Pilato akitaka kuwaridhisha umati, akawafungulia Baraba. Akampiga Yesu mijeledi kisha akamtoa ili asulibiwe.
16Askari walimwongoza hadi ndani ya ua (ule ulio ndani ya kambi) na walikusanyika pamoja kikosi cha askari.
17Wakamvika Yesu kanzu ya rangi ya zambarau, na wakasokota taji ya miiba wakamvika.
18Wakaanza kumdhihaki na kusema, “Salam, Mfalme wa Wayahudi!”

19Wakampiga kichwani kwa mwanzi na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake kwa kumheshimu.
20Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua ile kanzu ya rangi ya zambarau na kumvika mavazi yake, na wakamtoa nje kwenda kumsulibisha.
21Wakamlazimisha mpita njia kumsaidia, aliyekuwa anaingia mjini kutoka shamba. Aitwaye Simoni Mkirene (baba yake Iskanda na Rufo); wakamlazimisha kubeba msalaba wa Yesu.
22Askari wakampeleka Yesu mahali paitwapo Goligotha (maana ya tafsiri hii ni, Sehemu ya Fuvu la kichwa).
23Wakampa mvinyo iliyochanganywa na manemane, lakini hakunywa.
24Wakamsulibisha na wakagawana mavazi yake, wakayapigia kura kuamua kipande atakachopata kila askari.
25Yapata saa tatu asubuhi walipomsulibisha.
26Wakaweka juu yake ubao ulioandikwa shitaka, “Mfalme wa Wayahudi.”
27Walimsubisha pamoja na majambazi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine kushoto kwake.
28(Zingatia: Mstari huu, “Na maandiko yakatimia yaliyonena” haumo katika nakala za kale).
29Nao waliokuwa wakipita walimtukana, wakitikisa vichwa vyao wakisema, “Aha! wewe utakayevunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu,
30jiokoe mwenyewe na ushuke chini toka msalabani!”
31Kwa namna ile ile wakuu wa makuhani walimdhihaki wakisemezana, pamoja na waandishi na kusema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe.
32Kristo Mfalme wa Israel, shuka chini sasa toka msalabani, ili tuweze kuona na kuamini.” Na wale waliosulubiwa pamoja naye pia walimdhihaki.
33Ilipofika saa sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa tisa.
34Wakati wa saa tisa, Yesu alipiga kelele kwa sauti kubwa, “Eloi, Eloi, lama sabaktani?” ikiwa na maana “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?”
35Baadhi ya hao waliosimama waliposikia wakasema, “Tazama, anamwita Eliya.”
36Mtu mmoja akakimbia, akajaza siki katika sponji na kuiweka juu ya mti wa mwanzi, akampa ili anywe. Mtu mmoja akasema, “Ngoja tuone kama Eliya atakuja kumshusha chini.”

37Kisha Yesu akalia kwa sauti kubwa na akafa.
38Pazia la hekalu likagawanyika vipande viwili toka juu mpaka chini.
39Ofisa mmoja aliyekuwa amesimama akimwelekea Yesu, alipoona amekufa kwa jinsi ile, akasema, “Kweli huyu mtu alikuwa Mwana wa Mungu.”
40Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakitazama kwa mbali. Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu (mama yake Yakobo mdogo wa Yose), na Salome.
41Wakati alipokuwa Galilaya walimfuata na kumtumikia. Na wanawake wengine wengi pia waliambatana naye hadi Yerusalemu.
42Kulipokuwa jioni, na kwa kuwa ilikuwa siku ya maandalio, siku kabla ya Sabato,
43Yusufu wa Arimathaya alikuja pale. Alikuwa ni mjumbe wa Baraza anayeheshimiwa mtu anayeutarajia Ufalme wa Mungu. Kwa ujasiri akaenda kwa Pilato, na kuuomba mwili wa Yesu.
44Pilato akashangazwa kwamba Yesu tayari amekufa; akamwita yule afisa akamwuliza kama Yesu amekufa.
45Alipopata uhakika kwa afisa kwamba amekufa, alimruhusu Yusufu kuuchukua mwili.
46Yusufu alikuwa amenunua sanda. Akamshusha toka msalabani, akamfunga kwa sanda, na kumweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika mwamba. Kisha akalivingirisha jiwe mlangoni mwa kaburi.
47Mariamu Magdalena na Mariamu mama yake Yose waliona sehemu alipozikwa Yesu.