Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Zekaria

Zekaria 7

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Mwaka wa minne wa utawala mfalme Dario, siku ya nne ya mwezi wa Kisleu (ambao ni mwezi wa tisa), neno la Yahwe lilimjia Zekaria kusema.
2Watu wa Betheli wamemtuma Shareza, Regemu Meleki na watu wao kuomba mbele ya uso wa Yahwe.
3Wakaongea na makuhani waliokuwa katika nyumba ya Yahwe wa majeshi na kwa manabii; wakasema, “Je niomboleze katika mwezi wa tano kwa njia ya kufunga, kama nilivyofanya miaka mingi hii?”
4Ndipo neno la Yahwe wa majeshi liliponijia kusema,
5“Ongea na watu wote wa nchi na makuhani uwaambie, “Mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba katika hii miaka sabini, je kweli mlifunga kwa ajili yangu?
6Na mlipokula na kunywa, hamkula na kunywa kwa ajili yenu wenyewe?
7Je hayo siyo maneno aliyosema Yahwe kwa vinywa vya manabii wa zamani, mlipokuwa bado mnaishi Yerusalemu na miji ya kandokando yenye mafanikio na iliyokaa Negebu, na upande wa magharibi chini ya vilima?”
8Neno la Yahwe likamjia Zekaria kusema,
9“Yahwe wa majeshi asema hivi, 'Hukumuni kwa haki, uaminifu wa agano, na rehema. Kila mtu na amtendee hivi ndugu yake.
10Juu ya mjane na yatima, mgeni, na masikini - usiwanyanyase, na asiwepo miongoni mwenu anayepanga madhara yoyote dhidi ya mwingine mioyoni mwenu.
11Lakini waliyashupaza mabega yao na hawakujari. Waliziba masikio yao ili wasisikie.
12Waliifanya mioyo yao kuwa migumu kama mwamba ili wasiisikie sheria au neno la Yahwe wa majeshi. Alipeleka ujumbe kwa watu nyakati za zamani kwa Roho wake, kwa vinywa vya manabii. Lakini watu hawakusikia, hivyo Yahwe wa majeshi aliwakasirikia sana.
13Hata ikawa alipoita hawakusikia. Vilevile,” asema Yahwe wa majeshi, “wataniita, lakini sitasikiliza.
14Kwa maana nitawatawanya kwa upepo wa kisurisuri katika mataifa yote ambayo hawajawai kuyaona, na baada yao nchi itakuwa wazi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja atakayepita au kukaa katika hiyo nchi kwa kuwa wameigeuza nchi yao yenye kupendeza kuwa isiyofaa.