Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 9

Matendo 9:17-39

Help us?
Click on verse(s) to share them!
17Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, “Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu.”
18Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa.
19Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko.
20Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
21Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!”
22Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa.
23Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumwua Saulo.
24Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumwua.
25Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani.
26Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa, na hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi.
27Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila uoga kule Damasko.
28Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu.
29Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wasemao Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua.
30Wale ndugu walipogundua jambo hilo walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso.
31Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu.
32Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda.
33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Enea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza.
34Basi, Petro akamwambia, “Enea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako.” Enea akaamka mara.
35Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Enea, na wote wakamgeukia Bwana.
36Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima.
37Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakauzika katika chumba ghorofani.
38Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: “Njoo kwetu haraka iwezekanavyo.”
39Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonyesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai.

Read Matendo 9Matendo 9
Compare Matendo 9:17-39Matendo 9:17-39