Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 4

Matendo 4:7-28

Help us?
Click on verse(s) to share them!
7Waliwasimamisha mitume mbele yao, wakawauliza, “Ninyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?”
8Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu!
9Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima,
10basi, ninyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye ninyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka wafu.
11Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: Jiwe mlilokataa ninyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.
12Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.”
13Hao wazee wa baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu.
14Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu.
15Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha.
16Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba mwujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo.
17Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.”
18Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni ninyi wenyewe kama ni haki mbele ya Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii yeye.
20Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
21Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo.
22Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arobaini.
23Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.
24Waliposikia habari hiyo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo!
25Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, babu yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure?
26Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, ili kumwasi Bwana na Kristo wake.
27“Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye umemtia mafuta.
28Naam, walikutana ili wafanye yale ambayo ulikusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako.

Read Matendo 4Matendo 4
Compare Matendo 4:7-28Matendo 4:7-28