Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 3

Matendo 3:8-26

Help us?
Click on verse(s) to share them!
8Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.
9Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.
10Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.
11Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane.
12Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?
13Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.
14Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.
15Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.
16Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.
17“Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu.
18Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.
19Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu.
20Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.
21Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani.
22Kwa maana Mose alisema, Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe.
23Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.
24Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi.
25Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.
26Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake.”

Read Matendo 3Matendo 3
Compare Matendo 3:8-26Matendo 3:8-26