Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 27

Matendo 27:3-22

Help us?
Click on verse(s) to share them!
3Kesho yake tulitia nanga katika bandari ya Sidoni. Yulio alimtendea Paulo vizuri kwa kumruhusu awaone rafiki zake na kupata mahitaji yake.
4Kutoka huko tuliendelea na safari, lakini kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kwa kasi kutujia kwa mbele, tulipitia upande wa kisiwa cha Kupro ambapo upepo haukuwa mwingi.
5Halafu tulivuka bahari ya Kilikia na Pamfulia, tukatia nanga Mura, mji wa Lukia.
6Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani.
7Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo upepo haukuwa mwingi.
8Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo “Bandari Nzuri”, karibu na mji wa Lasea.
9Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo aliwapa onyo:
10“Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu.”
11Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo.
12Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike. Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi.
13Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakang'oa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na pwani ya Krete.
14Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao “Upepo wa Kaskazi” ulianza kuvuma kutoka kisiwani.
15Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo.
16Kisiwa kimoja kiitwacho Kanda kilitukinga kidogo na ule upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule mtumbwi wa meli.
17Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libya. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli ikokotwe na upepo.
18Dhoruba iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli.
19Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe.
20Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia.
21Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, “Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote.
22Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea.

Read Matendo 27Matendo 27
Compare Matendo 27:3-22Matendo 27:3-22