Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 19

Matendo 19:16-35

Help us?
Click on verse(s) to share them!
16Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
17Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.
18Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.
19Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha elfu hamsini.
20Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.
21Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.”
22Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia.
23Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo Njia ya Bwana.
24Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi faida kubwa.
25Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, “Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii.
26Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si tu hapa Efeso, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo.
27Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha.”
28Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: “Mkuu ni Artemi, wa Efeso!”
29Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo.
30Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia.
31Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimtumia Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo.
32Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao.
33Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu.
34Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!” Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili.
35Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, “Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni.

Read Matendo 19Matendo 19
Compare Matendo 19:16-35Matendo 19:16-35