Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 19

Matendo 19:10-26

Help us?
Click on verse(s) to share them!
10Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana.
11Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo.
12Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao.
13Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya, walisafiri huko na huko, wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: “Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri.”
14Watoto saba wa Skewa, Kuhani Mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo.
15Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?”
16Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
17Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.
18Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.
19Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha elfu hamsini.
20Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.
21Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.”
22Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia.
23Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo Njia ya Bwana.
24Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi faida kubwa.
25Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, “Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii.
26Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si tu hapa Efeso, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo.

Read Matendo 19Matendo 19
Compare Matendo 19:10-26Matendo 19:10-26