Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 17

Matendo 17:8-32

Help us?
Click on verse(s) to share them!
8Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu.
9Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao.
10Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi.
11Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonika. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli.
12Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.
13Lakini, Wayahudi wa Thesalonika walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu.
14Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea.
15Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo.
16Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu.
17Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano sokoni pamoja na wowote wale waliojitokeza.
18Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, “Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?” Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, “Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni.”
19Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, “Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia.
20Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani.”
21Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya.
22Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, “Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba ninyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana.
23Sababu yenyewe ni kwamba katika pitapita yangu niliangalia sanamu zenu za ibada nikakuta madhabahu moja ambayo imeandikwa: Kwa ajili ya Mungu yule Asiyejulikana. Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu.
24Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu.
25Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na anawapa kila kitu.
26Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi.
27Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu.
28Kama alivyosema mtu mmoja: Ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu, na tuko! Ni kama washairi wenu wengine walivyosema: Sisi ni watoto wake.
29Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu.
30Mungu alifanya kama kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu.
31Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka wafu!”
32Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, “Tunataka kukusikia tena juu ya jambo hili!”

Read Matendo 17Matendo 17
Compare Matendo 17:8-32Matendo 17:8-32