22Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, “Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba ninyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana.
23Sababu yenyewe ni kwamba katika pitapita yangu niliangalia sanamu zenu za ibada nikakuta madhabahu moja ambayo imeandikwa: Kwa ajili ya Mungu yule Asiyejulikana. Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu.
24Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu.
25Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na anawapa kila kitu.