Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 17

Matendo 17:17-30

Help us?
Click on verse(s) to share them!
17Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano sokoni pamoja na wowote wale waliojitokeza.
18Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, “Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?” Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, “Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni.”
19Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, “Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia.
20Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani.”
21Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya.
22Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, “Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba ninyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana.
23Sababu yenyewe ni kwamba katika pitapita yangu niliangalia sanamu zenu za ibada nikakuta madhabahu moja ambayo imeandikwa: Kwa ajili ya Mungu yule Asiyejulikana. Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu.
24Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu.
25Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na anawapa kila kitu.
26Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi.
27Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu.
28Kama alivyosema mtu mmoja: Ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu, na tuko! Ni kama washairi wenu wengine walivyosema: Sisi ni watoto wake.
29Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu.
30Mungu alifanya kama kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu.

Read Matendo 17Matendo 17
Compare Matendo 17:17-30Matendo 17:17-30