Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 16

Matendo 16:11-19

Help us?
Click on verse(s) to share them!
11Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.
12Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa.
13Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo.
14Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.
15Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.
16Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.
17Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.”
18Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.
19Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.

Read Matendo 16Matendo 16
Compare Matendo 16:11-19Matendo 16:11-19