Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 15

Matendo 15:1-21

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, “Kama hamtatahiriwa kufuatana na mapokeo ya Sheria ya Mose, hamtaweza kuokolewa.”
2Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee kuhusu jambo hilo.
3Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote.
4Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.
5Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, “Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata Sheria ya Mose.”
6Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa kuchunguza jambo hilo.
7Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, “Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia na kuamini.
8Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.
9Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.
10Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?
11Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.”
12Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.
13Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: “Ndugu zangu, nisikilizeni!
14Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.
15Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
16Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena.
17Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana.
18Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.
19“Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: tusiwataabishe watu wa mataifa wanomgeukia Mungu.
20Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa najisi kwa kutambikiwa sanamu za miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu.
21Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato.”

Read Matendo 15Matendo 15
Compare Matendo 15:1-21Matendo 15:1-21