Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 14

Matendo 14:3-20

Help us?
Click on verse(s) to share them!
3Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu.
4Watu wa mji huo waligawanyika: wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume.
5Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe.
6Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani,
7wakawa wanahubiri Habari Njema huko.
8Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa amelemaa miguu tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe.
9Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa,
10akasema kwa sauti kubwa, “Simama wima kwa miguu yako!” Huyo mtu aliyelemaa akainuka ghafla, akaanza kutembea.
11Umati wa watu walipoona alichofanya Paulo, ulianza kupiga kelele kwa lugha ya Kilukaonia: “Miungu imetujia katika sura za binadamu!”
12Barnaba akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme.
13Naye kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua mbele ya mlango mkuu wa mji, na pamoja na ule umati wa watu akataka kuwatambikia mitume.
14Barnaba na Paulo walipopata habari hiyo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa:
15“Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama ninyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo.
16Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda.
17Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha.”
18Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie.
19Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa.
20Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe.

Read Matendo 14Matendo 14
Compare Matendo 14:3-20Matendo 14:3-20