Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 13

Matendo 13:9-26

Help us?
Click on verse(s) to share them!
9Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi,
10akasema, “Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka.
11Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo.” Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze.
12Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.
13Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu.
14Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa.
15Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: “Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni.”
16Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: “Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni!
17Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu.
18Aliwavumilia kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani.
19Aliyaangamiza mataifa ya nchi ya Kanaani akawapa hao watu wake ile nchi kuwa mali yao.
20Miaka mia nne na hamsini ilipita, halafu akawapatia waamuzi wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samweli.
21Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa Saulo, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka arobaini.
22Baada ya kumwondoa Saulo, Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme wao. Mungu alionyesha kibali chake kwake akisema: Nimemwona Daudi mtoto wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote ninayotaka kuyatenda.
23Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu.
24Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa.
25Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.
26“Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.

Read Matendo 13Matendo 13
Compare Matendo 13:9-26Matendo 13:9-26